Matukio kadhaa yanaufanya mwaka 2014 kuwa wenye kumbukumbu ya
aina yake katika sekta ya elimu nchini. Fuatana na mwandishi kujua
matukio hayo ya kielimu yaliyoteka hisia za watu wengi kwa mwaka mzima.
Mfumo mpya wa madaraja ya ufaulu waibua mjadala
Februari 22, mwaka huu, Baraza la Mitihani la
Tanzania (Necta), limetangaza Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa kidato cha
nne wa 2013, huku ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 15.17 kupitia mfumo
mpya wa upangaji ambao ulipanua wigo wa alama na madaraja ya ufaulu.
Upangaji wa alama hizo ni A: 75-100, B+:60-74,
B:50-59, C:40-49, D:30-39, E:20-29 na F:0-19. Kabla ya mabadiliko hayo,
alama zilizokuwa zikitumiwa kupanga matokeo ya kidato cha nne zilikuwa
ni A:80-100, B:65-79, C:50-64, D:35-49 na F: 0-34.
Hata hivyo, wadau wengi wa elimu waliokosoa mfumo
huo akiwamo Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,a
aliyesema mabadiliko hayo yalilenga kuongeza ufaulu ili kuridhisha
wapiga kura kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Shule 10 bora 2013 zaporomoka
Julai 17, mwaka huu shule za sekondari zilizokuwa
kwenye orodha ya 10 bora katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2013,
zimeporomoka na shule isiyo maarufu ya Igowole kutoka mkoani Iringa
ilichomoza kutoka nafasi ya nane hadi ya kwanza mwaka huu.
Aliyekuwa kaimu katibu mtendaji wa Baraza la
Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema katika matokeo ya
mwaka jana, kati ya shule 10 zilizokuwa na watahiniwa zaidi ya 30, ni
shule nne pekee zimeendelea kuwamo katika kundi la shule 10 bora kitaifa
mwaka huu.
Shule zilizoporomoka mwaka huu ni Marian Girls
(Pwani) iliyokuwa ya sita mwaka huu wakati mwaka 2013 ilishika nafasi ya
kwanza. Shule zilizotoka patupu katika orodha hiyo mwaka huu ni Mzumbe
(Morogoro) iliyokuwa ya pili, Ilboru Arusha (ya nne) na Mtakatifu Mary
Mazinde Juu ya Tanga (ya sita).
Wizara yaifuta EMAC
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilisikia
kilio cha muda mrefu cha wadau wa elimu kuhusu kuwapo kwa vitabu visivyo
kuwa na viwango vilivyokuwa vikipewa ithibati na iliyokuwa Kamati ya
Kusimamia Vifaa vya Elimu (EMAC).
Septemba mosi, wizara ikaifuta kamati hiyo na kuhamishia majukumu yake kwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET)
Kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na wizara hiyo, TET kwa sasa
itakuwa na mamlaka ya kuchapisha vitabu na kuvisambaza kwa utaratibu wa
kitabu kimoja kwa kila darasa na kila somo kuanzia ngazi ya awali,
msingi, sekondari na vyuo vikuu.
Uamuzi wa kuifuta EMAC hasa baada mjadala mzito wa
kitaifa kuhusu ubora wa vitabu ulioibuliwa na Mbunge wa kuteuliwa,
James Mbatia ambaye Julai akiwa bungeni alisema vitabu vingi vina
maarifa yanayowapotosha wanafunzi.
Nusu wafaulu darasa la saba
Novemba 6, wazazi wengi walipata faraja baada ya
Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), kutangaza matokeo ya mtihani wa
darasa la saba mwaka 2014, yakionyesha kuwa zaidi ya nusu ya wanafunzi
waliofanya mtihani huo Septemba mwaka huu, walifaulu.
Matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa
Necta, Dk Charles Msonde, yalionyesha kuwa ufaulu uliongezeka kwa
asilimia 6.38 ikilinganishwa na mwaka 2013. Shule ya Twibhoki iliyopo
mkoani Mara ndiyo iliyoibuka kinara kitaifa kati ya shule 15,867
ikifuatiwa na shule za Mugini, Peace Land na Alliance zote za mkoani
Mwanza.
Hata hivyo, wadau walikosoa matokeo hayo wakisema
miongoni mwa waliofaulu wapo wanaoshindwa stadi za msingi za kusoma na
kuandika.
Tanzania yang’ara kusini mwa Afrika
Wakati wananchi wakiendelea kutafakari
kinachoendelea juu ya udhaifu wa elimu nchini, Desemba 9, mwaka huu
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco)
kupitia ripoti yake ya Elimu kwa Wote (EFA), lilitoa matokeo ya
kushangaza.
Ofisa mipango na mwakilishi wa Unesco nchini,
Zulmira Rodrigues, alisema tangu kuwekwa kwa malengo sita ya elimu kwa
wote mwaka 2000, Tanzania ilishavuka lengo la asilimia 57.1 kwa kupata
asilimia 72.2.
Kwa mujibu wa EFA, lengo la sita ni kushughulikia changamoto ya kujua kusoma na kuandika.
Necta yatangaza mfumo mpya
Tukio lililofunga mwaka lilijiri Desemba 13, mwaka
huu baada ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), kuanzisha mfumo
mpya wa kupanga matokeo ya kidato cha nne mwaka huu na ya kidato cha
sita mwakani, ambapo kwa sasa madaraja yatapangwa kwa wastani wa pointi
(GPA) badala ya jumla ya pointiMsonde alisema hayo katika mkutano wa wadau wa kampeni ya elimu kwa
watoto wa kike uliofanyika mkoani Dodoma. Alisema mfumo huo siyo mpya
kutumiwa na Necta kwa sababu umekuwa ukitumiwa katika kupanga matokeo ya
wanafunzi wa vyuo vya walimu. Alisema kuwa thamani ya madaraja itabaki
kuwa ilivyo ila kutakuwa na mfumo unaolingana na upangaji matokeo kama
ilivyo katika vyuo vya ualimu. Lengo la mfumo huo aliongeza kuwa ni
kuwezesha kuwa na mfumo unaofanana katika ngazi zote za elimu nchini.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment