Siku moja baada ya Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kuifungia
Kampuni ya Lino International kuendesha mashindano ya Miss Tanzania kwa
miaka miwili, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hashim Lundenga amesema hatua
hiyo imefikiwa kutokana na shinikizo kutoka kwa baadhi ya watu wenye
dhamira ya kuitoa kwenye mstari wa mafanikio sanaa ya urembo nchini.
Lundenga alisema jana uamuzi wa Basata ni
utekelezaji wa dhamira ya wachache walioamua kuhakikisha Miss Tanzania
inapotea kwenye ramani ya burudani nchini.
Lundenga alisema uamuzi huo wa upande mmoja,
haujaangalia mafanikio ya mashindano hayo kwa miaka 21 tangu kuanza
kwake na wala hatima yake baadaye.
“Niseme kweli, kwa mtu mwenye mapenzi ya kuona
sanaa ya urembo inasonga mbele kwa mafanikio, kamwe hawezi kuchukua
uamuzi wa kukomoa kama huu, ila kwa watu wachache walioamua kuharibu
taswira ya mashindano kwa sababu zisizo na uzito, wanaweza kufanya
hivyo,” alisema Lundenga.
Aliongeza: “Siko hapa kutaja majina ya watu
waliojipanga kuharibu mashindano haya, lakini kwa akili isiyohitaji kazi
kubwa kufikiria jambo rahisi kama hili, haiwezi kupata tabu kuamini
ukweli kwamba kuna watu nyuma ya uamuzi huu wa Basata.”
Lundenga alisema wameshangazwa na uamuzi huo wa
kufungiwa, kwani umekuja katika mazingira yasiyoeleweka ambayo
hayakuwapa fursa ya kujieleza.
“Tumefanya mashindano haya kwa mafanikio kwa miaka
zaidi ya 20, iweje leo tunapewa adhabu kubwa kiasi hicho kwa makosa
madogo,” aliongeza Lundenga.
Akifafanua, Lundenga alisema Novemba 21 mwaka huu,
walipewa barua ya onyo yenye vipengele vinne na kutakiwa
kuvishughulikia kwa ajili ya msimu wa mwakani, lakini Desemba 22 mwaka
huu walipewa barua ya kutakiwa kusimamisha mashindano.
“Kuna tatizo hapa. Leo unapewa barua ya onyo kabla
hujafanya chochote unapewa barua ya kusimamishwa tena bila hata kupewa
nafasi ya kujitetea. Ni aina gani ya uamuzi kama si kuwa na watu wenye
nia mbaya na mashindano haya,” alisema.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment