mabaki ya nyumba ya mzee ambayo ilichomwa kutokana na imani za kishirikina
Madai ya kuroga mvua, upigaji ramli, ugomvi ndani ya ndoa, tamaa
ya kurithi mali, ardhi na ng’ombe ni miongoni mwa mambo yanayoelezwa
kusababisha ongezeko la mauaji ya wazee vikongwe katika baadhi ya mikoa
nchini.
Shirika linalojishughulisha na haki za wazee la
Help Age International, limetaja sababu hizo kuwa ndizo zilizoendeleza
wimbi la mauaji hadi kufikia idadi ya wazee zaidi ya 4,612 kuuawa kutoka
mwaka 1998 mpaka 2014.
Anasema kwa mujibu wa ripoti ya Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu ya mwaka 2009, wanawake wazee 2,583 waliuawa katika
mikoa minane ikiwa ni wastani wa mauaji 517 kila mwaka.
“Takwimu za Mkoa wa Mwanza pekee, ambao ndiyo
ulikuwa na mauaji mengi nchini zilionyesha kuwa wanawake wazee 689
waliuawa kati ya mwaka 2002 na 2007 ikiwa ni wastani wa mauaji 140 kila
mwaka,” anasema Meneja wa Programu wa Help Age, Flavian Bifandimu.
Anasema taarifa kutoka Shinyanga pia zinatisha, kwani wanawake wazee 242 waliuawa kati ya Januari 2010 na Juni 2011.
Sababu za mauaji
Mwenyekiti Mtendaji kutoka asasi ya Maperele ya
Magu, Joseph Mandalo anasema mauaji ya wazee Mwanza na maeneo
yanayouzunguka mkoa, yalitokana na ugomvi wa kifamilia na ndoa.
“Mauaji ya wazee yana sababu nyingi, mara nyingi
yanaanzia katika migogoro ya familia na tatizo kubwa ni ardhi na mali.
Sasa inapofikia hatua wanazihitaji, wanatumia kigezo cha kwamba ni
mchawi ili wapate kirahisi,” anasema Mandalo.
Anaongeza: “Wengi wanatumia njia za mkato
kujipatia mali kwa kuondoa uhai wa wengine. Ukichunguza kwa umakini
utagundua kwamba mipango ya mauaji inafanywa na wanafamilia.’’
Mwenyekiti wa chama cha watu wanaoishi na Ukimwi
Wilaya ya Bukombe, Essau Malifedha anasema katika mila za Kisukuma, kuna
mambo kadhaa kama vile kuchelewa kwa mvua. Anasema zinapochelewa jamii
humhisi kikongwe yeyote kuwa ndiye aliyesababisha hali hiyo.
“Usukumani mvua zinapochelewa kunyesha, wanaamini
kwamba ni mwanamke mzee na moja kwa moja wanakimbilia kupiga ramli.
Wakati mwingine ni tamaa za mali, unakuta mzazi anamrithisha mali mtoto
akiwa mdogo, sasa wanapokua wanaona mzee hafi wanaamua kumuua ili
warithi,” anasema Malifedha na kuongeza kuwa mtazamo huo ni athari
itokanayo na ujinga.
Anaongeza kuwa mauaji kwa wazee yanatofautiana
kutoka eneo moja hadi jingine… “Ukiona shingo imekatwa mara moja unajua
ni kabila gani limehusika na mauaji, kama panga limekata zaidi ya mara
mbili ni kabila jingine vivyo hivyo na maeneo ya mwili na marehemu.”
Kubini Nkondo kutoka shirika la Nabroho Society For The Age
liliyopo Simiyu anasema uchawi una uhusiano na mauaji ya wazee wengi.
“Tunachokiona hapa mauaji ya wazee hayana uhusiano
na uchawi japokuwa wanaoua huweka dhamira hiyo, kwa kwani takwimu
hazipungui na kama ni kweli tungeona wamepungua.
“Kwa mfano, mwaka 2008 huko Magu- Chandulu kuna
mzee mmoja alikatwa mapanga, siku moja baadaye kuna watu walisikika
wakidaiana ujira klabuni,” anasema na kuongeza:
“Lakini kumbe walidhulumiana na hapo ndipo kijiji
kilipojua kumbe waliua kwa ajili ya mali na si uchawi waliomtuhumu.
Mwaka 2007, kuna mzee aliuawa kwa ajili ya kusuluhisha ugomvi wa
wanandoa, huko kwetu hakuna usawa kijinsia,” anasema Nkondo.
Sera ya Taifa ya Wazee
Bifandimu anahoji kwa nini imani hizi zinasababisha mauaji mengi ya wazee na bado hakuna mikakati mahususi ya kuwanusuru?
“Sera ya Taifa ya Wazee (Nap) ndiyo pekee
inayolaumu mila potofu ikiwa ni pamoja na mauaji ya wazee kwa tuhuma za
uchawi, lakini kwa bahati mbaya, sera hii bado haijatungiwa sheria.
Mkukuta inayoelekeza jinsi masuala ya wazee yatakavyoshughulikiwa bado
haijalishughulikia suala la mauaji ya wazee,” anasema.
Anasema Tanzania inazo sheria mbalimbali ambazo
zinalenga kuwalinda wazee kama raia wengine, lakini kesi nyingi
zinazohusiana na mauaji ya wazee zimekuwa zikiishia njiani kwa maelezo
kuwa hakuna ushahidi wa kutosha na hivyo kuendelea kuuawa kwa tuhuma za
uchawi.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment