Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
HALMASHAURI ya wilaya ya Hanang mkoani Manyara, imeunda kamati ya
ufuatiliaji utekelezaji wa maelekezo ya serikali kuhusu elimu bure
itakayowahusisha watendaji wa kata, wazazi, wakuu wa shule na wataalamu
wa elimu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Felix Mabula alisema hayo
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu
namna walivyojipanga kuhakikisha mpango wa elimu bure unafanikiwa.
Alisema, kuundwa kwa kamati hiyo kutasaidia ufuatiliaji wa karibu wa
kuhakikisha wazazi au walezi hawatozwi michango iliyokuwa nje ya
maelekezo ya serikali pamoja na kutekeleza waraka Namba 5 na 6 kuhusu
elimu bure.
Alifafanua kuwa, Halmashauri ina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa
waraka huo katika kuainisha majukumu ya wazazi, walimu, Bodi za Shule na
Kamati za Kata (WDC) na kufuatilia utozaji wa michango isiyoidhinishwa
na waraka huo.
Aidha, alisema kamati hizo zitahakikisha bodi za shule na wazazi
zinakutana mara kwa mara na kupanga matumizi sahihi ya namna
watakavyowapatia watoto wao chakula shuleni.
“Tunafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kuwa walimu wakuu pamoja na
bodi ya shule wanapata ufafanuzi kuhusu miongozo na waraka
ilivyoainishwa ili kuweza kusimamia majukumu yao vizuri,” alisema
Mabula.
Katika hatua hiyo alieleza kuwa Halmashauri ya wilaya ya Hanang
imepokea Sh 11,456,000 zikiwa ni fedha kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya
elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, huku wakipokea Sh 64,642
kwa shule za sekondari na shule za msingi ni Sh 49,918,000.
Naye Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya
ya Hanang, Omary Maje alisema, wametoa maelekezo kuwa mtoto asiachwe
kupelekwa shule hata kama mzazi wake hajachangia michango ya chakula
shuleni, kamati husika zina jukumu la kumfuatilia mzazi huyo kuhakikisha
anachangia chakula hicho.
Alisema, kupunguzwa huko kwa michango kumesababisha mwitikio mkubwa
wa mahudhurio ya wanafunzi kwani mpaka Januari 26, jumla ya wanafunzi
1,889 kati ya 2,386 waliochaguliwa sawa na asilimia 79.1, wameingia
shuleni.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment