Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wafungwa wanaotumikia vifungo mbalimbali katika
gereza kuu la Lilungu, mkoani Mtwara, wanakabiliwa na hali ngumu
kimaisha kutokana na kupewa chakula kibaya na huduma mbovu za vyoo hivyo
kutishia kuanzisha mgomo.
Taarifa ambazo Nipashe imezipata kutoka gerezani humo, zilizoelezwa
na wafungwa hao, zilisema tatizo la kupewa chakula kibovu limekuwa la
muda mrefu na uongozi wa gereza umekuwa hauchukui hatua kila ukielezwa.
Wafungwa hao (majina tunayo) walibainisha mambo sita
wanayolalamikia kuwa ni kupewa chakula kibovu na huduma mbaya za ndani
na kwamba hadi sasa bado wanatumia mtondoo na hakuna huduma ya matunda
hadi wakati wa msimu wa maembe tu.
Malalamiko mengine ni kukosekana kwa mboga za majani kutokana na
bustani ya gereza kubinafsishwa kwa mkuu wa gereza hilo ambaye
hulazimika kuuza mboga kwa gereza na kutokuwapo huduma ya nyama ambayo
wanapewa mare nne tu kwa mwezi.
Kutokana na hali hiyo, Januari 14, mwaka huu, wafungwa katika
gereza hilo walianza mgomo baridi baada ya kupikiwa mchele uliodaiwa
kuwa na wadudu (funza).
Walisema malalamiko hayo kila wanapowaeleza viongozi wao wamekuwa
wakijibu kuwa ni kwa sababu serikali haijawalipa wazabuni wanaotoa
huduma ya chakula.
Ofisa Habari Jeshi la Magereza, Deogratius Kazinja, alipoulizwa
alisema ofisi yake bado haijapokea malalamiko ya wafungwa hao na kwamba
taarifa rasmi za masuala hayo zinaweza kutolewa na viongozi wa juu wa
jeshi.
Kazinja alisema migomo ya wafungwa imekuwa ikijitokeza mara kadhaa
katika magereza lakini haisababishwi na uongozi wa magereza kushindwa
kutatua malalamiko yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara, Mussa Kaswaka,
alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia malalamiko hayo kwa sababu kwa
utaratibu wa jeshi hilo ni hadi apewe ruhsa ya kuzungumza na Kamishna
Jenerali wa Magereza.
“Mimi si msemaji wa Jeshi la Magereza. Nenda makao makuu kaonane
na Kamisha Jenerali wa Magereza halafu yeye ndiye atatoa maelekezo kama
niyatolee ufafanuzi,” alisema.
Juhudi za kumtafuta Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja,
hazikuzaa matunda jana. Hata hivyo Nipashe linaendelea kufanya jitihada
za kumtafuta ili kuzungumzia malalamiko hayo.
Migomo katika gereza hilo imekuwa ikijitokeza mara kadhaa mfano
mwaka juzi, wafungwa wanaotumikia waliitisha mgomo kushinikiza uongozi
wa gereza kuwatendea haki kama binadamu wengine kwa kuwapatia chakula
kizuri.
Kipindi hicho wafungwa hao walilalamika kuwa wanalishwa uji wa
chumvi, ugali na kunde ambazo hazijaungwa kila siku wakati wanastahili
kupewa uji wenye sukari, nyama, maziwa, matunda na mboga kama ratiba ya
chakula inavyoonyesha.
SOURCE:
NIPASHE.
0 comments:
Post a Comment