Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WANANCHI wa Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara, wamempiga askari polisi na kumpora bunduki aina ya SMG.
Tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana katika mnada wa Dosidosi,
wakati askari huyo alipokuwa akitaka kumwokoa mtuhumiwa mmoja aliyekuwa
akishambuliwa na wananchi mnadani hapo.
Polisi aliyeporwa bunduki hiyo, ametajwa kwa jina la PC Ginue anayefanya kazi katika Kituo cha Polisi Kibaya (Kiteto).
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa walioshuhudia tukio hilo, zinasema
polisi huyo alimwokoa mtu huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kuiba Sh
800,000.
Mmoja wa mashuhuda hao aliliambia MTANZANIA kuwa, mtuhumiwa huyo
ambaye hakupatikana jina lake, alimpora fedha hizo mmoja wa
wafanyabiashara wa ng’ombe na kukimbia nazo.
“Baada kupora fedha huyo mtu alikimbia nazo, lakini alikamatwa na kuanza kushambuliwa kwa silaha za jadi.
“Wakati mtuhumiwa huyo akishambuliwa na wananchi waliokuwa wamejaa
hasira, askari polisi waliokuwa mnadani hapo kwa ajili ya kuimarisha
ulinzi, walijitokeza na kutaka kumwokoa kwa kupiga risasi za moto
hewani.
“Baada ya kupiga risasi hizo, walisogea eneo la tukio wakiwa na gari
aina ya Noah na kumpakia mtuhumiwa kwenye gari haraka na kuondoka naye
wakielekea Kibaya ambako ndiko yaliko makao makuu ya Wilaya ya Kiteto.
“Wakati askari hao wanaondoka na gari hilo, PC Ginue alichelewa
kupanda gari hilo, kwa hiyo wananchi walimvamia na kuanza kumshambulia
kwa fimbo la silaha za jadi.
“Walipofanikiwa kumzidi nguvu, walimpora bunduki aliyokuwa nayo na kutokomea nayo kusikojulikana,” alisema mtoa taarifa huyo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Dosidosi, Juma Maganga, alithibitisha uwepo
wa tukio hilo na kusema waliopora bunduki hiyo wanatafutwa.
Pia, alisema wakati polisi huyo alipokuwa akishambuliwa, watu watatu
walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto kwa
matibabu zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka, pamoja na kuthibitisha uwepo
wa tukio hilo, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano, ili bunduki
iliyoporwa iweze kupatikana.
“Tukio hilo lipo, ila nawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kuipata
bunduki hiyo kwani kitendo cha kupora silaha ni kosa ambalo haliwezi
kuvumilika.
“Napenda pia kuwaamuru waliopora silaha hiyo, wairejeshe haraka kwani
msako mkali utafanyika hadi itakapopatikana na wahusika kutiwa mbaroni.
“Narudia tena hili halikubaliki hata kidogo, yaani raia anamnyang’anya askari silaha
kali kama SMG!
kali kama SMG!
“Hivi anapoichukua anaipeleka wapi, wairudishe haraka kwa sababu lazima watapatikana tu,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
CHANZO: MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment