MFUKO wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali (PSPF), umewataka wakazi
wa mkoa wa Manyara kutumia fursa ya kuchangia kwa hiyari na kujiwekea
akiba ya uzeeni kupitia ofisi iliyopo mkoani humo ili wapate mafao bora.
Akizungumza na wanahabari jana, Ofisa Mfawidhi wa PSPF mkoani humo
ambaye pia ni Meneja wa mfuko huo kwa mkoa huo, Said Ismail alisema,
baadhi ya wakazi hawautumii licha ya kupewa elimu ya uchangiaji wa
hiyari na umuhimu wa kujiwekea akiba ya uzeeni. Alisema, uchangiaji wa
hiyari hauko katika sekta rasmi pekee.
“Kwa sasa mfuko huu umepanua huduma zake hadi katika sekta isiyo
rasmi na kuwawezesha wafanyabiashara na wajasiriamali wengi kuchangia
bila kikwazo,” alisema.
Alisema, PSPF inatarajia kuanzisha fao la uzazi Julai mwaka huu,
ambapo mchangiaji atalazimika kuchangia kwa miaka miwili na kupata
asilimia 130 ya fedha alizochangia ikiwa ni pamoja na za mchango kutoka
katika mshahara wake.
Alisema hiyo ni kwa waajiriwa wa sekta rasmi. Alifafanua kuwa
kumekuwa na changamoto ya uchangiaji wa mfuko kimkoa ambapo jitihada
zaidi zinaendelea kufanywa ili kuelimisha jamii katika wilaya za
Simanjiro, Kiteto, Mbulu, Hanan’g, Babati kuona umuhimu wa kuchangia kwa
hiyari na kujiwekea akiba ya uzeeni.
Alitaja baadhi ya mafao yanayotolewa na mfuko huo kuwa ni mkopo wa
elimu, mikopo ya viwanja, mkopo wa nyumba, kuumia kazini, mirathi na
kustaafu.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment