Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Kwa
miaka mingi hapa nchini Tanzania, Kilimo kimetajwa kuwa uti wa mgongo
wa Taifa. Ikumbukwe kuwa miaka ya Sabini za mwanzoni kuliwahi kuwepo
kauli kuhusu kilimo iliyosema “Kilimo cha Kufa na Kupona”. Kauli hii
ililenga kuondoa njaa iliyokuwa inalikabili Taifa. Kwa miaka ya
hivi karibuni, serikali ikaja na Kauli Mbiu ya “Kilimo Kwanza”. Hizi
zote ni jitihada za kuinua kilimo ambacho kinategemewa na walio wengi
hapa kwetu.
Kilimo ni eneo la kipaumbele katika uchumi wa Tanzania licha ya kuwa kilimo nchini bado kinategemea kwa kiasi kikubwa mvua na hali ya hewa kwa ujumla .
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka ya hali ya hewa iliyotolewa na Mkurugenzi
Mkuu Dkt. Agnes Kijazi zinasema mvua za masika zimeshaanza katika
maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Mvua hizi
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Hata hivyo maeneo machache yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi
chini ya wastani.
Hali
ya unyevunyevu wa udongo inatarajiwa kuwa ya kutosheleza shughuli za
kilimo katika maeneo mengi.Hata hivyo, mvua za juu ya wastani
zinazoendelea kunyesha zinaweza kusababisha hali ya unyevunyevu wa
udongo kupita kiasi hivyo kuathiri mazao na hata kusababisha mafuriko na
kuharibu mazao.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, msimu wa mvua za Masika katika
kipindi cha miezi ya Machi hadi Mei, 2016 ni mahususi katika maeneo ya
Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na
Manyara), Pwani ya Kaskazini, (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani,
Morogoro-Kaskazini pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba), Kanda ya Ziwa
Victoria (Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga) na
kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani
hadi juu ya wastani kwa maeneo mengi ya ukanda huo isipokuwa maeneo ya
Kusini mwa ukanda huo yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya
wastani.
Kutokana
na mvua zinazoendelea kunyesha tahadhari imetolewa kwa wakulima wote
kuwa makini na mvua hizi za masika zinazoendelea kwani zinatarajiwa
kunyesha kwa wingi katika baadhi ya maeneo kulingana na uelekeo wa upepo
katika maeneo mengi ambayo yanayopata mvua za msimu wa masika.
Mwelekeo
wa mvua uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa hivi karibuni umezingatia
zaidi kipindi cha msimu(miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo
makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na
mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika
uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
Wakulima
wanashauriwa kuendelea na shughuli za kawaida za kilimo katika maeneo
yao ikiwa ni pamoja na kutumia mbinu za kuongeza uzalishaji, kupanda
mazao na miti kuzuia mmomonyoko wa udongo pamoja na kuzingatia ushauri
wa wataalam wa kilimo katika matumizi sahihi ya ardhi na mbegu. Hata
hivyo, katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini
ya wastani,upungufu wa unyevunyevu wa udongo unaweza kujitokea hususan
katika vipindi vya kukosekana kwa mvua. Wakulima waendelee kutafuta,
kupata na kuzingatia ushauri wa maafisa ugani katika kutekeleza shughuli zao.
Aidha
wataalamu wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine(SUA) katika
tafiti zao wametoa ushauri kuhusu namna bora ya kilimo cha baadhi ya
mazao kwa kuzingatia taratibu sahihi za kilimo za mazao hayo wakati huu
wa mvua za masika.
Ushauri kuhusu mtama
Mtama
unatarajiwa kukua vizuri wakati wa masika. Wakati wa kupanda mtama,
wakulima wanashauriwa kuanza utayarishaji wa mashamba kabla ya mvua.
Upandaji kavu (yaani upandaji kabla ya mvua) unapendekezwa sana kwa
mtama na ni bora wakulima wapande katika wiki za tatu na nne za Machi.
Wakulima wanaweza kuanza kupanda mtama katika mwezi wa pili (Februari)
kabla ya kupanda mimea mingine. Katika upandaji kavu, kina cha udongo
(yaani urefu wa shimo kwenda chini) kinahitajika kuwa sentimeta tano
ikilinganishwa na upandaji unyevu (yaani upandaji wakati udongo una
maji) ambapo kina kinahitajika kuwa kama sentimita mbili nukta tano
(2.5) hadi sentimita nne.
Wakulima
wanashauriwa kuweka mbolea vizuri kwa kuchanganya na udongo.Wakulima
wanashauriwa pia kupalilia angalau mara mbili wakati wa kukua kwa mimea.
Ushauri kuhusu Maharagwe
Ili kupata mazao
bora ya maharage, umwagiliaji wa maji ni muhimu. Kwa ajili ya mvua ya
kawaida au nyingi inayotarajiwa, uhifadhi wa maji ya mvua unahitajika
ili maji haya yatumike wakati wa mvua chache. Wakulima wanashauriwa
kutumia mbinu za umwagiliaji wa mifereji ya juu au chini wakati wa ukavu
kwa milimita 50 kwa wiki hadi mwisho wa msimu. Kwa kawaida, joto huwa
haina athari mbaya kwa maharage, kama kiwango kizuri cha maji kimo
mchangani.
Ushauri kuhusu Mahindi
Wakulima
wanashauriwa waanze kupanda mahindi kabla ya mwanzo wa mvua katika wiki
ya tatu au nne ya Machi. Mahindi yanafaa kupandwa punde tu hali ya
udongo na joto lake linapofaa kwani kuchelewesha upandaji kunaweza
kusababisha upungufu wa mavuno,kwa sababu mahindi yanahitaji unyevu bora
zaidi wa udongo wakati wa upandaji, wakulima wanashauriwa kutumia hatua
zinazofaa za kuhifadhi udongo.
Kutumia
mbinu za ukulima bora ni pamoja na upandaji miti na ukulima wa mseto
ambao unaweza kupunguza mmomonyoko wa udongo na kuongeza ubora wa maji
na udongo. Wakulima wanahimizwa wawe na mbinu ya kuondoa maji katika
maeneo yanayopata mvua nyingi ili kuzuia uharibifu wa mimea. Uchimbaji
wa mitaro ya kuondoa maji haya unaweza kuzuia mafuriko na pia mmomonyoko
unaopoteza udongo wa juu wenye rutuba. Kuchanganya mchanga na mbolea ya
shamba kunaweza kutayarisha udongo kwa unyonyaji wa maji.
Mamlaka
ya Hali ya Hewa imetoa wito kwa wakulima wote nchini kuzingatia ushauri
kutoka kwa wataalamu wa kilimo ili kuondokana na usumbufu utakajitokeza
katika msimu huu wa masika unaoendela nchini.
Mamlaka
ya hali ya hewa imewaomba watanzania kufuatilia utabiri wa saa 24, siku
10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa
Tanzania ili kujua hali inayotarajiwa kuwepo kwa kipindi chote hiki cha
msimu wa mvua za masika.
0 comments:
Post a Comment