Home » » BABATI WANUFAIKA KILIMO CHA UFUTA

BABATI WANUFAIKA KILIMO CHA UFUTA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
UFUTA 

Wakulima 397 wa vijiji vya Kakoi na Endadosh katika Wilaya ya Babati mkoani Manyara wamenufaika na kilimo cha ufuta baada ya kupatiwa mafunzo ya kilimo bora kwa kutumia kifaa maalumu cha kielektroniki.
Wakulima hao walipatiwa elimu hiyo na maofisa ugani kazi 10, ambao kati yao watano walikuwa Kijiji cha Kakoi na wengine watano kwenye Kijiji cha Endadosh.
Hayo yalielezwa na ofisa mazao wa mradi wa uzalishaji na masoko wa shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Mkulima iliyofanyika jana kwenye kijiji cha Endadosh, Kata ya Qash.
Elibariki alisema kwa kutumia vifaa hivyo, wakulima wengi wamenufaika navyo kwa kuwa sasa wanafuata kanuni bora za kilimo cha ufuta, ikiwemo kuandaa mashamba, mbegu bora na mbinu za kilimo bora kwa njia rahisi kuliko kuwatumia maofisa ugani.
“Lengo letu ni kila mkulima mwenye kifaa hicho, azifikie kaya za wakulima 50 kwa muda wa miezi sita, ili wanufaike na kilimo hicho na kutekeleza kauli mbiu ya “ufuta mafuta, mafuta hufuta jasho”,” alisema Elibariki.
Alisema kwa kutumia kilimo cha ufuta, wakulima wa Tarafa ya Mbugwe wilayani humo, wameweza kunufaika kiuchumi kwa kuwa awali wengi wao walikuwa na nyumba za tembe, lakini sasa wamejenga nyumba bora za kisasa.
Naye ofisa kilimo wa Mkoa wa Manyara, Coletha Shayo aliwataka wakulima kulima zao hilo kwa kuwa lina faida kubwa. Alisema ekari moja inaweza kutoa magunia sita yenye thamani ya Sh1.8 milioni.
“Katika kilimo chenye faida kwa mkulima kwa sasa ni kilimo cha ufuta kwani unaweza kutumia gharama za Sh200,000 hadi Sh300,000 kuandaa shamba, mbegu, kupanda, kupalilia na kuvuna na ukapata Sh1.8 milioni,” alisema Shayo.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa