Home » » Kijiji cha Boay chapitisha bajeti ya sh4.7milioni

Kijiji cha Boay chapitisha bajeti ya sh4.7milioni


Joseph Lyimo, Babati
WANANCHI wa Kijiji cha Boay Wilaya ya Babati Mkoani Manyara wameipitisha sh4.7 milioni ya bajeti ya mapato na matumizi ya kijiji hicho kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2012/13 kutokana na makusanyo ya ndani ya kijiji chao.

Akisoma bajeti hiyo Ofisa Mtendaji  wa kijiji hicho Alois Sanka alisema amehamia kijijini hapo bila kukabidhiwa fedha yoyote hivyo wanaanza kazi mpya bila salio lolote na kudai kuwa alichokabidhiwa na Halmashauri ya kijiji ni kitabu cha wageni tu.

Sanka alitaja vyanzo vya mapato ya kijiji hicho kuwa ni pamoja ushuru wa minara ya Vodacom inayolipia sh3.6 milioni, minara ya TTCL sh360,000 na Shirika la ugavi wa umeme (Tanesco) hulipa shilingi 234,000.

Alivitaja vyanzo vingine ni ushuru wa migahawa, maduka ya rejareja, mashine za kusaga na pombe za kienyeji pamoja na faini zinazotozwa wale wote wanaovunja sheria ndogondogo zilizopitishwa na mkutano mkuu wa kijiji.

Awali mmoja kati ya wanakijiji hicho, Matuta Kijuu alimuuliza Mwenyekiti wa kijiji hicho, Emanuel Kaji hatua zilizochukuliwa baada ya kuhama kwa aliyekuwa Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho bila kukabidhi nyaraka muhimu kwa mwenzake.

Akijibu swali hilo Kaji alisema kabla Ofisa Mtendaji huyo hajahama yeye na Halmashauri ya kijiji  walimbana ili akabidhi nyaraka zote lakini walipofika ofisini alikabidhi  kitabu cha wageni, meza moja na viti viwili akidai kuwa nyaraka zote za fedha zimeliwa na panya.

“Mbona nyaraka zilizoliwa na panya ni zile za fedha tu, ina maana hizo nyaraka za fedha zina utamu kushinda zingine au ni mambo ya kutufanya sisi wajinga, tunataka arudishwe hapa atuambie ziliko nyaraka na fedha zetu,” aliuliza Bruno Masanja.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho Kaji, alidai kuwa uchunguzi wa tukio hilo kwa Ofisa mtendaji wa kijiji kuhamishwa na kuondoka bila kukabidhi nyaraka za fedha ukikamilika atarudishwa alipo na kisha kufikishwa mahakamani.  
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa