Mussa Juma, Serengeti.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Hamisi Kagasheki, na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, jana walifika Serengeti kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete,kufuatilia tukio la majambazi kuvamia kambi ya kitalii ya Moivaro iliyopo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Majambazi hao walivamia kambi hiyo na kuwaua watu wawili ambao ni mtalii Eric Brewelmans Raia wa Uholanzi na Meneja Msaidizi wa hoteli hiyo, Renatus Benard kwa kuwapiga risasi.
Licha ya mauaji hayo, majambazi hayo pia yalimjeruhi kwa kumkata panga mke wa Erick, Annelnes Brewelmans na kupora vitu vyenye thamani ya mamilioni ya fedha, zikiwepo kamera, nguo na vitu vingine, kwa watalii wengine zaidi ya 40 toka nchi za Ufaransa,Hispania, Marekani, Denmark na China.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Nchimbi alitoa salamu za pole kwa wafiwa, akiwepo balozi wa Uholanzi na kutoa wito kuanzia sasa hoteli zote za kitalii katika hifadhi za Taifa kuwa na ulinzi wa uhakika wa bunduki.
Alisema Serikali haiwezi kuvumilia kuona vifo vya watu, vinatokea katika mazingira ambayo yangeweza kuzuilika hasa kwa kuimarisha ulinzi katika mahoteli na Kambi za utalii.
Naye Waziri Kagasheki, licha ya kutoa pole, alihoji wamiliki wa kambi ya Moivaro mahusiano baina ya Kambi hiyo na utalii, kijiji cha Rubanda na Jumuiya ya Uhifadhi jamii WMA.
“haiwezekani watu wapite kijijini hapa na kuingia kambini na kupora kuua na kujeruhi watu hapa lazima kuna tatizo”alisema Kagasheki.
Hata hivyo, Meneja wa Kambi hiyo, Joseph Goshashi alisema kundi la majambazi hao, lilivamia kambi hiyo majira ya saa nne usiku na kuanza kupita kila chumba kupekuwa wageni.
Alisema walipofika chumba cha Eric aliyekuwa na mkewe, aliwaomba watoke nje, lakini badala yake walimpiga risasi kifuani na kisha kumpiga panga mkewe.
Hata hivyo, Meneja huyo, alisema walishindwa kukabiliana na majambazi hao, kutokana na kuwa na silaha na wao walinzi wao hawana silaha.
Hata hivyo Kamanda wa polisi mkoani Mara, Simon Sillo hata hivyo, alisema kambi hiyo, imekuwa na matatizo kwani walipaswa kuwa na silaha na tayari waliagizwa kufanya hivyo.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment