Home » » SERIKALI YALAUMIWA KUAJIRI WALIMU WASIO NA WITO

SERIKALI YALAUMIWA KUAJIRI WALIMU WASIO NA WITO


na Lucy Ngowi, Mbulu
BAADHI ya walimu wilayani Mbulu, Manyara, wameilaumu serikali kwa kuajiri walimu wapya ambao wamekuwa wakijali zaidi maslahi binafsi badala ya wito wa kuwafundisha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima wilayani hapa, walisema walimu wanaoajiriwa hawapo tayari kufundisha masomo ya hisabati, Kiingereza na Sayansi kwa kuwa hawana msingi mzuri.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Harka, Joseph Hando alisema kwa sasa taaluma imechuja kwa kuwa walimu waliopo wapo kimaslahi zaidi.
“Sehemu kubwa ya walimu wa zamani ilikuwa ni kujitolea tofauti na ilivyo sasa, walimu hao wamekuja kupata ajira tu. Taaluma nayo imechuja,” alisema Hando.
Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Sanubaray, Debora Msuya, alisema ufundishaji wa walimu wanaotoka vyuoni hivi sasa ambao wanajulikana kama wa dot.com ni tatizo kwa kuwa wanaandaliwa kwa kulipuliwa.
Alisema katika ufundishaji wa darasa la kwanza na la pili, inatakiwa awekwe mwalimu aliyetulia na si hao wa kulipuliwa kwa kuwa, hawana muda wa kumfundisha mtoto mpaka aelewe.
Wakati huo huo, Ofisa Elimu wa Sekondari katika halmashauri hiyo, Michael Handu, alisema kuna haja kwa serikali kufanya marekebisho katika vyuo vya ualimu kwa kuwa kuna tatizo.
Aliongeza walimu wanaopokewa wanakuwa hawana nia ya dhati ya ualimu, kwani baadhi yao hawafanyi kazi ipasavyo wanaangalia masilahi zaidi.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa