na Lucy Ngowi, Hanang-Manyara
WINGI wa watoto katika darasa moja unasababisha mwalimu kushindwa kumsaidia mwanafunzi mmoja mmoja, hali inayochangia baadhi kumaliza shule wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Jorodom, iliyopo Kata ya Ganana katika Halmashauri ya Hanang, Salvatory Manyama, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia sababu zinazowafanya wanafunzi wamalize shule za msingi wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
“Kila darasa lina wanafunzi zaidi ya 80 na vyumba ni vidogo hata ukiweka madawati hayatoshelezi. Pia hali hiyo inakuwa ni tatizo kwa mwalimu kumpitia mtoto mmoja baada ya mwingine na kumsaidia,” alisema.
Kwa upande mwingine, alisema katika darasa la awali lililopo katika shule hiyo lina wanafunzi 128, idadi ambayo ni kubwa, kwani kwa kawaida darasa linatakiwa kuwa na wanafunzi wasiozidi 25.
Alizitaja sababu nyingine zinazochangia watoto kutokujua kusoma na kuandika kuwa ni mwamko mdogo kwa wazazi na watoto katika suala la elimu, serikali kutokujali walimu kwa kuwapa upendeleo unaostahili, pamoja na muundo mzima wa utungaji wa mitihani.
Chanzo: Tanzania Daimav
0 comments:
Post a Comment