Home » » MWANAMKE ASAKWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI

MWANAMKE ASAKWA KWA TUHUMA ZA MAUAJI

Na Malima Lubasha, Serengeti
MKAZI wa Kitongoji cha Nyamturumwa, wilayani Serengeti, Rhobi Muhumbwa (26), anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua shemeji yake, Muhiri Muhumbwa (40), kwa kumchoma kisu.

Polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo walisema lilitokea Julai 29, 2012, saa nne usiku na inadaiwa alimchoma kwa kutumia kisu alichokinunua siku hiyo, kwa lengo la kumuua mwanamke mmoja kwa tuhuma za kutembea na mume wake.

Akielezea zaidi tukio hilo, Katibu wa Baraza la Jadi wa Kata hiyo, Peter Waitacho, alisema kabla ya mtuhumiwa huyo hajafanya unyama huo alinunua kisu na kukinoa kwa lengo la kumuua mama huyo anayetuhumiwa kutembea na mume wake.

Alisema siku ya tukio mtuhumiwa huyo alifika eneo la nyumbani kwa mwanamke huyo anayetuhumiwa kutembea na mumewe, lakini hakufanikiwa kumuona baada ya kumvizia kwa muda mrefu hali iliyomfanya aondoke katika eneo hilo.

“Baada ya mwanamke huyo kumvizia bila mafanikio aliamua kwenda nyumbani kwa shemeji yake ambaye baada ya kumuona kwake muda huo aliamua kumshushia kipigo kwa kuacha mifugo yenyewe bila muangalizi.

“Baada ya kuona kipigo alichopewa na shemeji yake kinazidi kuwa kikali, aliamua kuchomoa kisu na kumchoma nacho shemeji yake kifuani, hali iliyomfanya kuanguka chini na kupoteza uhai hapo hapo,” alisema Waitacho.

Alisema baada ya mwanamke huyo kutenda unyama huo aliamua kwenda nyumbani kwa mwanamke aliyekuwa akimtuhumu kutembea na mumewe, kwa lengo la kumuua lakini hakufanikiwa kutokana na mwanamke huyo kukimbia na kujifungia ndani.

“Alitoka na kisu chake hadi kwa yule mama anayemtuhumu kuwa na uhusiano na mme wake, naye alipomuona alikimbilia ndani. Mwanamke huyo alitoa tambo nyingi akimtaka atoke nje lakini hakutoka, hali iliyomfanya mwanamke huyo kuondoka,” alisema Waitacho.

Alisema mtuhumiwa huyo alichukua Sh 280,000 na kuondoka na alikutana na mme wake njiani na kumdanganya kuwa mwanaye mmoja anaumwa.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa