Home » » SINTOFAHAMU: Hatma ya Michezo mkoa wa Manyara

SINTOFAHAMU: Hatma ya Michezo mkoa wa Manyara


Asalaam aleykum wapenzi wasomaji wa Ohayoda katika "kijiwe" chetu hiki cha SINTOFAHAMU ambako tunakutana kila siku ya Alhamisi tukijadili mada mbalimbali ambazo aidha zinafumbiwa macho na mamlaka husika au zinaacha maswali mengine ambayo yanaibua hali ya SINTOFAHAMU ya kuwa na maswli mengi kuliko majibu japo hakuna wa kuyajibu lakini tunaendelea kujiuliza.

Leo tunajadili hatma ya michezo katika mkoa wa Manyara hususani mchezo wa riadha ambao ni mchezo pekee ulioweza kuiletea nchi yetu sifa katika medani ya kimataifa. SINTOFAHAMU ni kwa nini michezo inazidi kudidimia katika mkoa wa Manyara? Na Je mamlaka husika zinafanya jitihada kufufua michezo katika mkoa huu?


John Steven Akhwari, 1968

Wiki iliyopita katika makala ya Shujaa Wetu tulimzungumzia John Steven Akhwari jinsi alivyoweza kuiletea nchi yetu sifa hadi mchango wake kutambuliwa na kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kuwa mjumbe wa heshima katika mashindano ya Sydney ya mwaka 2000 na yale ya Beijing 2008 (unaweza kusoma zaidi kwenye 

Leo hii Akhwari yupo nyumbani kwake Mbulu kasahaulika, hajulikani na anaonekana hana faida. Wenzetu huko nje (ya Tanzania) wanamthamini sana kiasi cha hata kutunga wimbo maalum kwa ajili yake pamoja na kutengeneza filamu (documentary) kwa ajili ya ushujaa wake alioufanya mwaka 1968 huko Mexico City, Mexico. Je mamlaka husika katika mkoa wa Manyara, hasa idara zenye dhamana ya michezo, zimefanya jitihada zozote kuhakikisha kuwa wanamichezo hawa kwanza wanaenziwa na wanatumiwa ili kuhamasisha michezo kwa watoto wa leo?

Manyara ilizalisha wanariadha mahiri nchi, lakini leo hii imekuwa ni historia. Sintofahamu waliko Francis Naali na Zebedayo Bayo na Sintofahamu kama kuna juhudi zozote zinazofanyika kutafuta warithi wa nafasi zao. Sintofahamu kama tumeshawahi kujua hazina kubwa tuliyonayo kwa kuwa na watu kama Filbert Bayi, ambaye siyo tu alikuwa bingwa wa dunia katika marathon bali aliweka REKODI YA DUNIA iliyodumu kwa zaidi ya miaka 30 bila kuvunjwa. Sintofahamu!


Sintofahamu kama Filbert Bayi angepewa fursa ya kupita katika shule zetu akahamasisha vijana, akielezea jinsi alivyoweza tena enzi zile hadi kuwa bingwa wa dunia leo hii tungekuwa na akina Filbert Bayi wangapi, SINTOFAHAMU

Filbert Bayi 
Sintofahamu kama hata wahusika wanafahamu Gidamis Shahanga anaishi wapi na kama wanarekodi zozote, Sintofahamu
Sintofahamu kwa nini hakuna mashindano yoyote ya riadha katika mkoa mkoa wetu, hasa katika enzi hizi zenye udhamini wa hali ya juu.


Mchezo wa riadha unatumia gharama ndogo sana kuliko michezo mingine, ndio tunahitaji viwanja vya kisasa, sawa kabisa lakini akina Filbert Bayi hawakuwa navyo pia lakini wakawa mabingwa wa dunia.
Sintofahamu kama akina Bayo, Naali amefikia hapo alipo kwa juhudi zake mwenyewe au amepewa msaada wowote.


Sintofahamu kama viongozi wetu wa mkoa na wilaya zake zote wanaelewa fursa zitakazoambatana kama wataanzisha mashindano ya riadha ya kimkoa kuibua vipaji. Tumeona wanariadha kutoka mkoa wetu wakishiriki na kushinda mashindano ya Kilimanjaro Marathon, Sintofahamu kama hata juhudi zao zinathaminiwa au basi kama juhudi zinafanywa kuhakikisha wanaibuka wanariadha wengi watakaouwakilisha vyema mkoa wetu.


Twende mbele turudi nyuma, mchezo wa soka si "wetu" na haujawahi kuwa wetu, sisi letu ni riadha n tunaweza riadha, sintofahamu kama "wakubwa" hasa waliopo kule Babati wanalitambua hili. tumeshuhudia katika mashindano ya soka ya kombe la Taifa ya kila mwaka, timu ya mkoa wa Manyara inavyoaibisha na kutolewa katika hatua za awali, sintofahamu kwa nini juhudi zile haziwekwi kwenye riadha.


Japo hali ya Sintofahamu inazidi kutanda kila sehemu katika sekta ya michezo hasa riadha, bado hatujachelewa kufanya jambo kwa ajili ya vijana wetu. Riadha inaweza kuwa moja ya ajira kubwa sana na kuinua uchumi wa nchi yetu na kuupa mkoa wetu sifa kubwa. Naamini wahusika watachukua hatua stahiki na kuelekeza juhudi zao kwenye riadha. Tuwatafute kina Steven Akhwari na Filbert Bayi, kwanza tuwape heshima wanayostahili ili wawe chachu kwa vijana wetu watamani kuwa kama wao. INAWEZEKANA!



Chanzo: http://ohayoda.blogspot.com

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa