Home » » KIONGOZI MBIO ZA MWENGE AUGUA GHAFLA

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE AUGUA GHAFLA

Na Eliya Mbonea, Ngorongoro
KIONGOZI wa mbio za Mwenge mwaka huu, Kapteni Honest Mwanossa, ameugua ghafla, hatua iliyomfanya ashindwe kufungua miradi na kuweka jiwe la msingi katika baadhi ya miradi ya maendeleo.

Akiwa katika siku ya sita ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru katika wilaya za mkoa wa Arusha, Kapteni Mwanossa alijikuta akipata tatizo la afya na kulazimika kupatiwa huduma ya kwanza katika Zahanati ya Oloirobi aliyokuwa ameifungua.

Baada ya kupatiwa matibabu, kiongozi huyo, aliungana na msafara kuelekea Kijiji cha Mokila, kwa ajili ya kugawa mifugo na kuweka jiwe la msingi katika jengo la hosteli za baraza la wafugaji Ngorongoro.

Hata hivyo, kiongozi huyo hakuweza kuendelea na ratiba kutokana na hali kuzidi kubadilika.

Baada ya Mwenge kuwasili katika Shule ya Sekondari ya Embarway, kwa ajili ya kuzindua miradi kadhaa na kuweka jiwe la msingi, kiongozi huyo hakuonekana.

Miradi iliyokuwa ifunguliwe katika shule hiyo, ilikuwa ni kuweka jiwe la msingi katika madarasa matatu ya kidato cha tano na sita, kuona mradi wa Sensa, maoni ya Katiba mpya, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na ugonjwa Ukimwi.

Chanzo kimoja, kililiambia MTANZANIA kuwa kiongozi huyo, alikuwa amelazwa katika Zahanati ya Enduleni.

Akiwa zahanati kwa ajili ya matibabu, shughuli zake zilifanywa na mmoja wa vijana wanaokimbiza Mwenge kitaifa. Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawalali, alilazimika kutoa taarifa kwa wananchi kwamba Kapteni Mwanosa alikuwa na udhuru maalumu.

Hata hivyo, ulipofika wakati wa chakula cha usiku, ambako Mwenge ulilala katika Kijiji cha Enduleni, Kapteni Mwanossa aliibuka na kuwahakikishia wananchi kuwa afya yake ipo fiti.

Akizungumza na wakimbiza Mwenge kutoka mkoa na wilayani, waliokuwa wakiongozwa na DC Wawalali, Kapteni Mwanossa aliwashukuru NCCC kwa juhudi kubwa wanazoendelea kuzifanya za kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Mwenge wa Uhuru jana, ulikabidhiwa kwa viongozi wa Mkoa wa Mara na Mkuu wa Mkoa, Magessa Mulongo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa