ZAIDI ya vijana 200 wa kijiji cha Gawidu, wilaya ya
Hanang, mkoani Manyara, wamesusia kujiunga na mafunzo ya mgambo kutokana na
kile walichodai kwamba hawaoni faida ya mafunzo ya jeshi hilo.
Baadhi ya vijana hao ambao ni kati ya vijana 700
walioandikishwa kujiunga na mafunzo hayo, walikuwa wamebeba mabango yenye
ujumbe wa maneno yanayotaja sababu za kutoshiriki mafunzo hayo kuwa ni pamoja
na jeshi hilo kutokuwa na ajira.
“Mafunzo ya mgambo hatuyataki kwa sababu kwanza
hatujaomba, pili hamna ajira rasmi na tatu hatujashirikishwa kwenye hayo
maandalizi ya kufanya mgambo,” alisema Ali Musa Shaban.
Hata hivyo baadhi ya vijana hao walisema kwa sasa
wananchi wa kijiji hicho hawana amani kutokana na viongozi wao kuwagawa huku
wakiwa hawataki kuumaliza mgogoro wa shamba lililokuwa mali ya Nafco.
“Viongozi hawafai kwa sababu hawataki kutusikiliza
sisi kwani ndugu mkurugenzi alikuja akasema kwamba hakuna shughuli yoyote ya
maendeleo ambayo inatakiwa kuendelea kwenye kijiji hiki kama hakuna amani,
tunashangaa sasa hivi tunadaiwa tukafanye mgambo kule wakati huku hatuna amani
je, tukiondoka hapa tukiacha mama zetu na baba zetu wavamiwe na watu
tutafanyaje?” alihoji Baraka Ntandu mkazi wa kijiji cha Gawidu.
Akizungumzia malalamiko ya vijana hao, mwenyekiti
wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya ya Hanang ambaye pia ni mkuu wa wilaya
hiyo, Christina Mndeme, alikiri kundi hilo la vijana kugomea mafunzo hayo na
chanzo cha mgomo huo ni uchochezi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment