MFANYABIASHARA maarufu katika mji mdogo wa Galapo, wilayani Babati, Mkoa
wa Manyara, Walter Kanda (31), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa
kuwa majambazi alipokwenda kumuokoa baba yake, John Kanda (62), aliyevamiwa
nyumbani kwake.
Katika uvamizi huo licha ya kumuua mfanyabiashara huyo, watu hao
pia waliiba vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na bunduki aina ya Rifle iliyokuwa
ikimilikiwa na Kanda na kutokomea nayo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda ya Polisi Mkoa wa Manyara,
Akili Mpwapwa, alisema uchunguzi unaendelea kuhusiana na tukio hilo ili
kuwabaini wahusika kama hawana mahusiano na majangili wanaotafutwa.
“Tukio la mauaji ni tukio kubwa na linahitaji uchunguzi makini ili
kujiridhisha na wote wanaotuhumiwa kabla ya hatua nyingine za kisheria kufuatwa
kwani mbali na mauaji hayo kuna silaha imeibwa, pia kuna migogoro ya mashamba,
lakini kule pia yapo matukio ya uwindaji haramu, hivyo inahitaji uchunguzi wa
kina kujiridhisha,” alisema Mpwapwa.
Habari za ndani zinasema kuwa tayari kuna watu kadhaa wanashikiliwa
kuhusiana na tukio hilo akiwamo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha
Endadoshi, Kata ya Qash, Luka Bunye (CCM) kwa tuhuma za kuhusika katika
tukio hilo.
Pamoja na mwenyekiti huyo pia wapo wakulima wenzake, Everest Joachim,
mkazi wa Kijiji cha Halah na Jumanne Manja wa Qash Mwisho.
Kamanda huyo alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 8, mwaka huu, saa 5:30
usiku.
Habari zaidi zimeeleza kuwa kabla ya tukio hilo, Kanda (62), ambaye ni
baba yake marehemu alitoka ndani kwenda chooni na ghafka alikutana na kundi la
watu waliomrushia risasi kwa kutumia silaha inayosadikiwa kuwa ni bastola huku
wengine wakimkata mapanga.
“Risasi hiyo ilipiga ukuta wa choo, nikamrukia mmoja nikawa najikinga
naye ili yule mwenye bastola asinipige, tukaburuzana hadi mlango wa choo.
Nikamsukumia kwa wenzake, nikapata nafasi nikaingia chooni na kufunga mlango,”
alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kuingia chooni, watu hao walianza kusukuma
mlango huku akipiga kelele za kuomba msaada, ghafla mtoto wake alitoka nje
na kuwatambua wale watu ndipo walipompiga risasi ya ubavuni na kuanguka.
“Watu hao waliingia ndani na kuchukua bunduki yangu aina ya Riffle,
fedha na nyaraka zinazohusu mashamba yangu, ambapo tayari majirani walikuwa
wameanza kutupa mawe juu ya nyumba yangu, hivyo wakakimbia kusikojulikana,”
alisisitiza.
Eneo hilo limegubikwa na migogoro ya mashamba kwa muda mrefu,
inayosababisha hofu baina ya wakazi wa maeneo hayo.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment