WAFUGAJI zaidi ya 100 wa jamii ya Kibarbeig wa
Kitongoji cha Gidaburuku, Kijiji cha Mulbadau wilayani Hanang’, Mkoa wa
Manyara, wanaendelea kuishi porini katika shamba la Gawal baada ya kuchomewa
nyumba na maboma yao kupisha ugawaji wa ardhi.
Nyumba hizo zipatazo 24 za wafugaji hao zilianza
kuteketezwa wiki iliyopita na kikundi cha wakulima wa kijiji hicho, wakiongozwa
na viongozi wa serikali ya kijiji na askari wa Kutuliza Ghasia (FFU).
Kuteketezwa makazi hayo ya wafugaji
kumefanyika wiki moja tu tangu Mkuu wa Mkoa, Erasto Mbwilo, kuwataka
waondoke kwenye makazi yao kabla ya kuondolewa kwa nguvu ili kupisha
ugawaji wa ardhi hiyo ya shamba la Gawal yenye ukubwa wa ekari 4,030.
Wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa
uteketezaji huo ukiendelea, wafugaji hao walisema licha ya kuchomewa makazi yao
pia wamechomewa vyakula na baadhi ya mifugo yao kutawanyika.
Veronica Gidaregek akizungumza akiwa nje ya nyumba
ya familia yake iliyoteketezwa, alisema kundi la wakulima likiongozwa na
Mwenyekiti wa kijji hicho, Christopher Panga, walivamia nyumba hiyo na kuanza
kuichoma moto bila hata kumruhusu kutoa mali zake.
“Mimi sina pa kwenda, nitalala hapa nje na watoto
wangu wawili, kwani wamenichomea nyumba na mali zangu zote na mume wangu
amesafiri,” alisema Gidaregek.
Nao Mwale Lwagei na Hiyi Hando, walisema wachomaji
hao huku wakilindwa na polisi walichoma maboma yao bila hata kuwaelekeza wapi
pa kwenda kama nia ni kugawa upya maeneo hayo kwa wananchi wote wa kijiji
hicho.
“Kwa kaka yangu, Gidabugai Masungu, walichoma
nyumba ndani akiwemo mzazi na nusura wamteketeze kwa moto mtoto mmoja mchanga
ambaye tulimuokoa,” alisema Lwagei.
Diwani wa Kata ya Basotu, Samweli Kawoga,
alithibitisha kuchomwa makazi na kueleza kuwa shughuli hiyo ilisimamiwa na
viongozi wa kijiji cha Mulbadau.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Erasto Mbwilo, jana
alisema hakuagiza viongozi wa kijiji hicho wala polisi kuchoma makazi hayo.
“Mimi kwenye ule mkutano nilichoagiza ni wale
waliovamia eneo la shamba la Gawal kuondoka ili kupisha ugawaji wa ardhi hiyo,
sasa kama kuna watu wamechoma makazi hayo ni makosa na mimi sina taarifa,”
alisema.
Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Akili
Mpwapwa, alisema polisi hawakutumwa kusimamia uchomaji wa makazi bali kusimamia
upimaji wa ardhi ya eneo hilo ili baadaye igawanywe.
Kwa zaidi ya miaka miwili wafugaji hao wamegoma
kuhama katika shamba hilo la Gawal wakishinikiza kupewa kipaumbele katika
kupewa ardhi hiyo, kwa kuwa wao ndio walifukuzwa na serikali ilipochukua ardhi
hiyo kuanzisha Shirika la Taifa la Chakula (NAFCO) mwaka 1980.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment