Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam, John Mnyika
Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam, John Mnyika amependekeza
kusitishwa kwa muda kwa uwindaji wa tembo nchini kama njia muhimu ya
kupambana na vitendo vya ujangili.
Mnyika ambaye alikuwa akizungumza kama Mjumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, alitoa
mapendekezo hayo juzi baada ya kutembelea Hifadhi ya Tarangire.
“Tatizo hili (la ujangili) ni kubwa ni vizuri
Tanzania ikaiga nchi nyingine duniani…Tupige marufuku kwanza kwa muda
uwindaji wa tembo ili kuziba kabisa mianya na visingizio,” alisisitiza
Mnyika.
Mnyika aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kwa
hali ilivyo sasa, wapo tembo wanaowindwa kwenye vitalu na hiyo inaleta
mkanganyiko kati ya uwindaji haramu na uwindaji halali.
Halikadhalika Mnyika alitumia fursa hiyo kuitaka
Serikali kuwataja na kuwashtaki kortini vigogo wa ujangili kabla ya
kuanza kwa awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza Ujangili (OTU II).
“Kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ni vizuri wale
vigogo wa ujangili waliotajwa kwa ujangili wakatajwa kwa majina ili
wachukuliwe hatua...Tunataka itakapoanza awamu ya pili isiwalenge tu
wananchi,” alisema Mnyika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira, James Lembeli alisema, wanyama kama Nyumbu wapo
hatarini kutoweka kama hatua za makusudi hazitachukuliwa.
Alisema kutoweka kwa wanyama hao kutasababishwa na
wimbi kubwa la kuzibwa kwa mapito ya wanyama (corridor) kati ya hifadhi
na hifadhi na hivyo wanyama hao kushindwa kwenda kuzaliana.
“Hali hii ni hatari kwa maisha ya hifadhi zetu
hasa hizi za kaskazini…Mfano wakati hii Tarangire inaanzishwa kulikuwa
na Corridor (mapito) tisa, leo tunapozungumza zimebaki tatu tu,”alisema.
Lembeli alisema endapo ikitokea njia hizo
zikazibwa kabisa, wanyama watajikuta wanabakia eneo moja na kushindwa
kwenda maeneo ya kuzaliana, hivyo watazeeka na kufa bila kuongezeka.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment