JUMLA
ya vijiji vipatavyo 20 vya Wilaya ya Mbulu Mkoa wa Manyara, ambavyo
vilikuwa vikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji, vinatarajia kunufaika
na huduma hiyo baada ya kuwekwa kwenye mpango wa mradi kumaliza tatizo
hilo.
Hayo yamebainishwa juzi na Mhandisi wa maji wa halmashauri ya
wilaya hiyo, Bw. Ramadhan Mulungu, kwenye baraza la madiwani, ambapo
alisema kuwa vijiji 20 vinatarajia kupata huduma hiyo mwezi Julai mwaka
huu, na hivyo wananchi kuondokana na tatizo hilo la maji.
Bw.
Mulungu alisema vijiji hivyo 20 vitakavyonufaika na huduma hiyo ya maji
vipo kwenye kata za Geterer, Endamilay, Masqaroda, Gunyoda, Tumati,
Muday, Masieda, Maghang, Maretaduna Endagaw.
Alisema, serikali
kupitia wizara ya maji imeweka mpango wa miaka mitano wa kuhakikisha
matatizo ya maji yanakwisha kupitia mpango wa awamu ya pili wa
upatikanaji wa maji vijijini kwa kutenga vijiji 20 kwa kila wilaya
kupata maji.
"Kupitia fursa hiyo ya kila vijiji 20 kwenye wilaya
zote nchini kupata maji, wananchi wa Wilaya ya Mbulu ambao walikuwa
wanakabiliwa na tatizo hilo au kufuata maji umbali mrefu watapata huduma
hiyo," alisema Bw. Mulungu.
Hata hivyo, Naye Diwani wa kata ya
Daudi, Bw.Paul Sulle aliwataka watumishi wa idara ya maji wilayani humo
,kufanya tafiti na kutoa uzito kwenye maeneo yanayopatikana maji, hivyo
kunufaisha idadi kubwa ya watu.
"Tatizo la maji lipo, hivyo kutokana
na hali ilivyo hivi sasa inatakiwa mfanye utafiti kwanza kabla ya
kufanikisha mpango huo, kwani kuna baadhi ya maeneo kuna maji ya kuchota
hivyo mkitoa kipaumbele wengi watanufaika na huduma hiyo," alisema
Bw.Sulle.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment