Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KATIBU
Mtendaji wa Baraza la Biashara la Taifa la Biashara (TNBC), Raymond
Mbilinyi, ameshauri Mkoa wa Manyara kufanya kazi kwa bidii na kuongeza
ushirikiano miongoni mwao ili kuzidi kusaidia kujenga mazingira bora ya
biashara na uwekezaji mkoani humo kwa maendeleo ya mkoa na nchi nzima
kwa ujumla.
Mbilinyi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na
waandishi wa habari mkoani humo mwishoni mwa wiki. Alisema wajumbe
hawana budi kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano zaidi ili kukuza
shughuli za biashara na uchumi.
"Napongeza baraza hili ambalo
limejumuisha wajumbe kutoka sekta ya umma na binafisi kwa kuonesha
mwamko mkubwa wa kufanya kazi," alisema.
Alisema biashara na
uwekezaji katika mazingira ya sasa unategemea ushirikiano wa sekta ya
umma na binafsi kukaa pamoja na kujadili namna ya kuendeleza biashara na
uwekezaji.
Alisema wajumbe wa baraza wanatakiwa kujadili kwa uwazi
vikwazo na njia ya kuyatatua na pale inaposhindikana yatasababisha
kupatiwa suluhisho katika ngazi ya taifa.
Alisema Desemba mwaka 2013
ulifanyika mkutano wa saba wa Baraza la Biashara la Taifa, chini ya
Uwenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete na ajenda zilikuwa tatu ikiwemo
Watanzania kushiriki katika uchumi, Matokeo Makubwa Sasa na kuboresha
mazingira ya biashara.
Alisema ajenda hizo zinatakiwa kufanyiwa kazi katika ngazi ya mkoa ili kupata ufanisi zaidi.
"Nitafurahi
kuona baraza la mkoa huu mkiendeleza hili kwa nguvu ili kufikia malengo
yanayokusudiwa," alisisitiza Mbilinyi. Akifafanua zaidi alisema ngazi
ya mkoa na wilaya zikiweka mazingira bora ya biashara itasaidia
wafanyabiashara kushiriki vema na kuwa hayo yote yanategemea zaidi
wajumbe hao wa baraza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la
Biashara la Mkoa wa Manyara, ambaye pia Mkuu wa Mkoa huo, Elaston
Mbwilo, alisema sekta ya umma itahakikisha inashirikiana vizuri na sekta
binafsi kupitia baraza hilo.
"Sekta ya umma itafanya kazi kulingana
na jinsi tunavyojadili hapa katika kukuza biashara na uwekezaji,"
alisema Bw. Mbwilo. Alisema mkutano huo ulikuwa ni fursa kubwa kwao
kuzungumzia masuala yanayolenga kujenga biashara na uwekezaji wa mkoa
wao.
Pia alitoa mwito kwa baraza hilo kuziunganisha sekta ndogo za
ufugaji na kilimo ambazo ndizo shughuli kuu za mkoa huo, lakini zimekuwa
hazina uhusiano mzuri. Aliagiza kufanyika kongamano ambalo
litawaunganisha wafugaji kwa kuwa hawana umoja kama ilivyo kwa wakulima.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment