Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KUSHUKA kwa kiwango cha elimu nchini kumechangiwa kwa kiasi kikubwa
na upungufu wa baadhi ya vitendea kazi shuleni pamoja ari ya
ufundishaji ya walimu kupungua kutokana na mishahara midogo
wanayolipwa.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mkuu wa Shule ya Sekondari
Wakisimiri, Emmanuel Kisongo, kwenye mkutano wa Kanda ya Kaskazini
Magharibi ulioshirikisha mikoa ya Arusha na Manyara.
Kisongo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule
za Sekondari (Tahossa), alisema ili kufanikisha malengo ya mpango wa
serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa upande wa sekta ya elimu,
serikali inatakiwa kuboresha maeneo hayo.
“Matokeo makubwa sasa hayawezi kuja hivi hivi, yanatakiwa yaandaliwe.
Shule zinafanana, lakini changamoto zake zinatofautiana, hasa katika
suala la miundombinu ya ufundishaji, hivyo serikali inatakiwa kuangalia
pale penye mapungufu paboreshwe,” alisema Kisongo.
Alitoa wito kwa serikali kuangalia suala la siasa shuleni na kusema
kuna baadhi ya wanasiasa, hasa madiwani wamekuwa na tabia ya kuingilia
taratibu za shule hadi kukwaruzana na walimu kwa maslahi yao binafsi.
“Ninaweza kusema siasa imebeba kila kitu katika jamii zetu kwani kuna
wakati wanasiasa hao, hasa madiwani wamekuwa wakiingilia kazi za
walimu kwa lengo la kulinda wapiga kura wao, wanatumia shule kama
jukwaa la siasa na sio sehemu ya kutolea taaluma,” alisisitiza.
Awali akifungua mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Khalid Mandia,
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo, aliwataka wakuu
hao wa shule kutowakatisha tamaa walimu wageni wanaopangiwa kufundisha
katika shule zao, na badala yake kuwatia moyo ili waweze kufanya kazi
zao kwa ari na kufanikisha azma ya Matokeo Makubwa Sasa.
Chanzo:Tanzania
0 comments:
Post a Comment