Na Bertha
Mollel – Manyara
Mgogoro
mkubwa umeibuka juu ya nani mmiliki halali wa timu ya Tanzanite FC ambao ni
mabingwa wa mkoa wa manyara, baada ya
wadau wa kandanda katika mji mdogo wa mererani kuvutana na mfanya biashara
mdogo wa madini ya tanzanite Charles Andrew “Mnyalu” anayeihudumia timu hiyo kwa sasa.
Hali hiyo
imejitokeza baada ya Tanzanite kufanya
vibaya katika ligi ya mabingwa wa mikoa iliyomalizika hivi karibuni ambapo Tanzanite waliondolewa katika ligi hiyo
kutokana na wachezaji wake kumdunda mwamuzi na baadaye kushindwa kulipa
faini waliyopangiwa hali iliyosababisha Tanzanite FC kuenguliwa katika ligi
hiyo.
Wadau hao
kutoka mirerani wamemshutumu Mnyalu kuimiliki timu kinyume na makubaliano ya
kuitafutia wafadhili na badala yake kujitangaza kuwa ni mmiliki wa timu hiyo
baada ya kukabidhiwa leseni na cheti cha usajili wa timu.
Walisema
kuwa kutokana na kujitangaza huko Mnyalu
amekuwa akipata misaada mbalimbali na kujinufaisha kwa misaada hiyo anayopata kwa mwamvuli wa
kuwa mmiliki wa Tanzanite FC wakati si kweli bali alikuwa kama mfadhili tu.
Kocha wa
timu hiyo, Ally Matimbwa anayesimama kwa niaba ya viongozi halali wa Tanzanite
FC amesema yeye ndiye mmliki halali wa Tanzanite na kosa kubwa walilolifanya ni
kumkabidhi Mnyalu timu na baadaye kuwageuka na kuihodhi timu hiyo moja kwa moja.
“Sisi ndie
wamiliki halali wa timu ya Tanzanite FC na tulikuwa tunashindwa kumudu baadhi
ya gharama ambapo tuliamua kutafuta wafadhili na kumpata Mnyalu ambapo kosa
kubwa tulilofanya ni baadae kumuamini sana na kumpatia document za timu hali
ambayo sasa anatamba kuwa timu ni yake”
Akizungumzia
mgogoro huo mmiliki wa sasa wa Tanzanite FC, Charles Andrew “mnyalu” akionyesha kushangazwa na tuhuma hizo alisema
kuwa kuna baadhi ya watu wanatumika kumchafua baada ya kuona maendeleo ya timu
ya Tanzanite kutoka wilayani hadi sasa inatisha katika ngazi ya taifa.
“Hizo ni
kelele tu za watu kwa lengo la kunichafua baada ya kuona timu inapaa angani
kutoka wilaya, mkoa na sasa taifa, ndio
maana kelele nyingi zinaibuka ila kama ujuavyo dua la kuku haliwezi kumpata
mwewe ndivyo hivyo na mimi wala kelele hizo hazitanirudisha nyuma kuihudumia
timu hiyo na nazidi kusema kwa herufi kubwa kuwa mimi ndie mmiliki halali wa
timu na anaepinga ajitokeze” Alijitamba Mnyalu.
Hata hivyo
jitihada za Tanzania daima kutaka kujua juu ya nani hasa mmiliki wa timu ya Tanzanite
FC ulifika hadi chama cha soka wilayani simanjiro (SIDFA) ambapo nao
walithibitisha kuwa Charles Andrew “mnyalu” ndiye mmiliki halali wa timu hiyo.
Akizungumza
na Tanzania daima, Katibu wa SIDFA, Zefania Simon alisema kuwa Mnyalu ndie mwenye vyeti vya usajili na
amekuwa akiihudumia timu hiyo tangu ligi ya wilaya,mkoa na sasa ligi ya
mabingwa wa wilaya ambapo ameshangazwa na hali ya baadhi ya watu kujitangaza
kuwa wao ndio walikuwa wamiliki wa timu ya Tanzanite FC.
Kufuatia
madai hayo, Zefania ametoa onyo kali kwa
watu hao wanaojiita wamiliki wa timu ya Tanzanite FC na kuwataka kufuata taratibu halali kwa mujibu
wa katiba ya chama juu ya uhalali huo.
Alisema kuwa
watu hao hadi sasa wakiitwa kwenye vikao
na mikutano ya SIDFA wamekuwa hawajitokezi na badala yake kulaumu na kutoa
shutuma za kunyang’anywa timu nje ya vikao halali hali ambayo ni kinyume na
sheria na taratibu za soka.
Uongozi wa
chama cha soka mkoani Manyara (MARFA)
kupitia mwakilishi wa vilabu Fortunatus Kalewa umetoa tamko kuwa hawawezi
kuzungumzia umiliki wa timu hiyo kwani wao hawana timu bali timu ni za wilaya
hivyo tamko litakalotolewa na wilaya ya simanjiro ndio tamko halali na tayari
wilaya ya simanjiro imeidhinisha kuwa timu ya Tanzanite FC ni mali halali ya
Charles Andrew “mnyalu”
0 comments:
Post a Comment