Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MSANII wa Bongo fleva na mchimbaji madini wa Kampuni ya Tanzanite
One katika mji mdogo wa Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara,
Moses Komba (28), amenusurika kufa kwa kujipiga risasi kwa kile
kilichodaiwa aliihifadhi vibaya bastola kwenye pochi yake.
Akizungumza na Tanzania Daima, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Manyara, Deusdedit Nsimeki, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 3:30
usiku katika eneo la Kazamoyo, Kata ya Endiamtu.
Nsimeki alisema kuwa msanii huyo ambaye pia anajishughulisha na
shughuli za uchimbaji wa madini ya tanzanite, alijipiga risasi ya paja
la kulia na kutokea la kushoto kwa kutumia bastola yake aina ya
‘Brown’.
“Tukio hilo la kujipiga risasi limetokea kwa bahati mbaya, kwani
Komba hakuiweka vizuri silaha hiyo ambayo hadi hivi sasa inashikiliwa
kwenye kituo cha polisi Mirerani, baada ya baba yake kuisalimisha,”
alisema Nsimeki.
Alisema bado hawajabaini chanzo halisi cha tukio hilo, japo inadaiwa
kuwa Komba alichomoa bastola hiyo baada ya gari lake kugongwa ubavu wa
kulia na gari jingine ambalo halikutambulika mara moja.
Alisema Komba alikuwa barabarani eneo la Kazamoyo akiendesha gari
lake aina ya Toyota Celica lenye namba za usajili T 725 CLK, akagongwa
na gari jingine, ndipo akataka kutoa bastola hiyo, ghafla ikafyatuka na
kumpiga mguuni.
Nsimeki alisema majeruhi huyo amelazwa kwenye hospitali ya Arusha
Lutheran Medical Center (ALMC), Seliani, kwa ajili ya kupatiwa matibabu
na hali yake inaendelea kuwa nzuri.
Aliongeza kuwa hadi hivi sasa hawajabaini gari lililogongana na gari
la Komba, ila wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku
wakiishikilia silaha hiyo na gari lake kwa ajili ya uchunguzi.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment