Home » » WADAU MANYARA WGOMBANIA TIMU

WADAU MANYARA WGOMBANIA TIMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MGOGORO umeibuka juu ya umiliki halali wa timu ya Tanzanite FC ambayo ni mabingwa wa Mkoa wa Manyara, baada ya wadau wa soka katika mji mdogo wa Mirerani kuvutana na mfanyabiashara mdogo wa madini ya tanzanite, Charles Andrew ‘Mnyalu’ anayeihudumia kwa sasa.
Hali hiyo, imejitokeza baada ya Tanzanite FC kufanya vibaya katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL), iliyomalizika hivi karibuni, ambapo iliondolewa baada ya wachezaji wake kumdunda mwamuzi na baadaye kushindwa kulipa faini.
Wadau hao, wamemshutumu Mnyalu kuimiliki Tanzanite FC kinyume na makubaliano ya kuitafutia wafadhili na badala yake kujitangaza kuwa ni mmiliki baada ya kukabidhiwa leseni na cheti cha usajili wa timu.
Walisema kuwa kutokana na kujitangaza huko, Mnyalu amekuwa akipata misaada mbalimbali na kujinufaisha kwa mwamvuli wa kuwa mmiliki wa Tanzanite FC, wakati alikuwa kama mfadhili tu.
Kocha wa timu hiyo, Ally Matimbwa, alisema yeye ndiye mmliki halali wa timu hiyo, na kosa kubwa walilolifanya ni kumkabidhi Mnyalu timu na baadaye kuwageuka na kuihodhi moja kwa moja.
“Sisi ndio wamiliki halali wa Tanzanite FC na tulikuwa tunashindwa kumudu baadhi ya gharama, ambapo tuliamua kutafuta wafadhili na kumpata Mnyalu. Kosa kubwa tulilofanya ni baadaye kumuamini sana na kumpatia ‘documents’ za timu, hali ambayo sasa anatamba kuwa timu ni yake,” alisema.
Kwa upande wake, Mnyalu akionyesha kushangazwa na tuhuma hizo, alisema kuwa kuna baadhi ya watu wanatumika kumchafua baada ya kuona maendeleo ya Tanzanite FC kutoka wilayani hadi sasa inatisha katika ngazi ya taifa.
“Hizo ni kelele tu za watu kwa lengo la kunichafua baada ya kuona timu inapaa angani kutoka wilayani, mkoani na sasa taifa, ndiyo maana kelele nyingi zinaibuka, ila kama ujuavyo dua la kuku haliwezi kumpata mwewe, ndivyo hivyo na mimi wala kelele hizo hazitanirudisha nyuma kuihudumia timu na nazidi kusema kwa herufi kubwa kuwa, mimi ndiye mmiliki halali wa timu na anayepinga ajitokeze,” alitamba Mnyalu.
Tanzania Daima ilipiga hodi Chama cha Soka Wilaya ya Simanjiro (SIDFA), ambako Katibu wake, Zefania Simon, alithibitisha Mnyalu ndiye mmiliki halali wa timu hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Zefania alitoa onyo kali kwa watu hao wanaojiita wamiliki wa timu hiyo na kuwataka kufuata taratibu halali kwa mujibu wa katiba ya chama, juu ya uhalali huo.
 Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa