Ukosefu wa umoja au vyama vya michezo wilayani Hanang'
iliyoko mkoani Manyara, imeelezwa kama chanzo cha kudorora kwa michezo
mingi katika wilaya hiyo ingawa washabiki wapo wa kutosha na wenye
vipaji kadhalika.
Akizungumza na Tanzania daima, Ofisa Utamaduni wa
Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ James Surumo alisema kuwa wilaya hiyo
haina vyama vya michezo mingi, ila chama cha soka wilaya ya Hanang’
(HDFA) ndicho kipo hai na viongozi wake wa wilaya ambao wanasimamia
kandanda pekee hali ambayo michezo mingine inakosa nafasi kutokana na
kukosa hamasa.
Alisema kuwa wakati Serikali inaandaa sera ya michezo
ingepaswa iende sambamba na vyama vya michezo husika vinavyopaswa
kuzisimamia, endapo Hanang' kungekuwa na viongozi wa vyama hivyo vya
michezo wilayani humo, wanamichezo wangepiga hatua na kupatia sifa
wilaya hiyo.
Alisema kwenye wilaya hiyo, vijana wengi wanapenda kucheza
michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa wavu, pete, kikapu, riadha na
mingineno ila kutokana na ukosefu wa viongozi wa vyama hivyo vipaji
hivyo hufa.
“Vipaji vingi vinashindwa kuendelezwa kutokana na
kutosimamiwa ipasavyo hivyo hufa kabla ya kutumika ila viongozi hao
wangekuwa na vyama hivyo Hanang’ tungepiga hatua kubwa kwenye michezo,”
alisema Surumo.
Miaka iliyopita wilaya ya Hanang’ ilibahatika kuwa na
wanariadha wengi mahiri, akiwemo mwanariadha wa kimataifa, Gidamis
Shahanga ila hivi sasa vipaji vipya vimeshindwa kuibuliwa na kutowepo
kwa wanaridha wapya.
0 comments:
Post a Comment