Home » » FAHAMU HAPA JUU YA KILIMO BORA CHA UFUTA NA CHUKUA MAAMUZI SASA KULIMA ZAO HILI

FAHAMU HAPA JUU YA KILIMO BORA CHA UFUTA NA CHUKUA MAAMUZI SASA KULIMA ZAO HILI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

UFUTA   (Sesamum indicum)

UTANGULIZI
         Ufuta (simsim/sesame) ni zao la kibiashara ambalo mbegu zake zina kiasi kikubwa cha mafuta kiasi cha asilimia 45 hadi 55.Na zao hili linaweza kulimwa maeneo mengi ya Afrika mashariki  na Tanzania.Ni zao ambalo linatowa mafuta yenye thamani kubwa na hivyo kulifanya zao bora la biashara.

HALI YA HEWA  INAYOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA

 Zao hili linawezwa kulimwa katika maeneo yanayopata mvua kidogo.Maeneo ya ukanda wa chini  usawa wa bahari hufaa zaidi kwa kilimo cha ufuta.Pia nyanda za juu ambazo ni chini ya mita 1500 hufaa kwa kilimo cha ufuta.Mfano kwa Tanzania unaweza Ukalima ufuta katika mikoa ya Morogoro,Lindi,Manyara,Dodoma,Iringa.


UDONGO UNAOFAA KWA KILIMO CHA UFUTA

Ufuta ustawi vizuri katika maeneo yenye udongo mwepesi mweusi na usiotuamisha maji,udongo tifutifu ni mzuri kwa kilimo cha ufuta,Pia ufuta unawezwa kulimwa katika udongo wowote lakini usiotuamisha maji.Ufuta hufa haraka kama maji yatatuama kwa muda mrefu shambani.

AINA ZA UFUTA

Kuna aina kuu mbili za mbegu za ufuta:

1) MBEGU ZA ASILI
     Wakulima wengi hupanda mbegu za asili, mbegu ambazo zilianza kulimwa miaka mingi iliyopita.Mbegu hizi nyingi zina mavuno kidogo na huchukua muda mrefu kukomaa Huchukua siku 140 hadi 180.

2) MBEGU ZA KISASA
     Mbegu hizi zinakomaa kwa muda mfupi na hutowa mavuno mengi, wastani wa kilogram 500 hadi 800 kwa ekari kama shamba litaandaliwa litapandwa na litatunzwa vizuri.Mbegu hizi huchukua siku 105 hadi 140 kukomaa.Mfano wa mbegu hizi ni Naliendele 92,Lindi 202,Ziada 94 na Mtwara 2009.

UPANDAJI WA UFUTA

Shamba la ufuta ni budi likatuliwe na kulimwa vizuri kabla ya kupanda,hata hivyo pia unaweza kupanda bila kukatua lakini mavuno yatapungua kidogo.Inashauriwa kupanda ufuta kwa mistari kwa vipimo vifuatavyo.Sentimeta 50 kwa 10 au 50 kwa 20 kama utapanda kwa kutumia mistari ya kuchimba vijifereji vidogo katika mstari na kudondosha mbegu hizo katika vifereji hivyo (Drilling method) na kwa kuacha mche mmoja mmoja kwa kila shina.
Pia sentimeta 50 kwa 30  au 60 kwa 30 kwa kuacha miwili kwa kila shina. Kwa Mbegu ya Asili Unaweza Kupanda kwa sentimeta 70 kwa 30 kwa Kuacha Miwili kwa Kila shimo.Fukia mbegu kwa sentimenta .2.5 hadi 5.

MUDA WA KUPANDA

Muda mzuri wa kupanda ufuta ni mwanzoni mwa msimu wa kilimo  yaani Mwishoni mwa mwezi Desemba hadi katikati kwa mwezi Januari.

MATUMIZI YA MBOLEA

Ufuta ni zao ambalo halihitaji matumizi makubwa ya Mbolea.Japokuwa hustawi zaidi katika udongo wenye rutuba ya kutosha.Kama utapanda katika ardhi isiyo na rutuba ya kutosha basi unaweza kutumia mbolea kiasi kidogo Mbolea kama vile UREA na BUSTA.

MATUNZO NA PALIZI

 Miche ya ufuta ni midogo na laini sana hivyo inahitaji palizi mapema hasa katika kipindi cha majuma manne ya kwanza .Pia katika kipindi hiki unatakiwa kupunguza miche iliyosongamana.Kadri utavyochelewesha palizi na kupunguzia mimea mapema ndivyo unavyoifanya mimea isikuwe vizuri na kujipunguzia kipato chako.

MAGONJWA YA UFUTA

Magonjwa makuu ya ufuta ni madoa ya majani na kuoza matawi na shina.Zuia magonjwa haya kwa Kupanda  mbegu bora  na kwa kutokupanda ufuta katika ardhi inayotuamisha  maji,pia itawezekana kubadilisha shamba usilime  ufuta katika shamba lililolimwa msimu uliopita.


WADUDU WANAOSHAMBULIA UFUTA

  Kuna wadudu wengi wanaoshambulia ufuta kama vile vibaruti (Ambao hushambulia hatua ya mwanzo kabisa ya miche iliyoota ya ufuta  ambapo vibaruti hula majani ya mwanzo ya mmea mara tu yanapojitokeza).Pia Aphidi hushambulia ufuta kwa kufyonza maji katika majani ya mimea hivyo kupelekea kukauka kwa majani ya mmea.
  Pia wapo funza wa majani ambao hula majani ya mimea na pia hufunga majani ya ncha ya mimea na kuzuia ukuaji wa matawi wa mimea,wadudu hawa ni hatari zaidi kwani wanazuia kutengenezwa kwa vitumba vya ufuta.
  Kuzuia vibaruti,kabla hujapanda mbegu yako changanya na dawa ya tunza au gaucho.Pia panda mbegu bora na fanya mzunguko mazao shambani.Wadudu wengine wakijitokeza tumia dawa kama karate,dimethoate.Twigathoate,duduall,duduba  na dawa nyingine za wadudu kabla wadudu hawajasababisha madhara makubwa shambani.

UVUNAJI

  Ufuta uliokomaa tayari kwa kuvunwa utaonesha mabadiliko ya majani yake na shina na matawi yatabadilika  rangi yake na kuwa njano au kahawia au yataanza kukauka,pia vitumba vya mwanzo vitaanza kubadilika rangi yake na kuanza kukauka hivyo utatakiwa ukate ufuta mapema kabla vitumba havijakauka na kupasuka.Vuna ufuta wako kwa kukata matawi ya ufuta  na kuyafunga katika matita ya saizi inayokufaa ila yasiwe matita makubwa sana ambayo hayatakauka katikati kwa urahisi yasimamishe matita yako kuelekeza juu kisha acha yakauke kwa wiki mbili hadi nne kutegemea na ukali wa jua.vitumba vikisha kauka na kupasuka tandika mkeka au turubai na yageuze matita yako katika mkeka na turubai hapo ufuta utamwagikia katika mkeka au turubai lako,kuupata ufuta unaokwama katika matita piga piga kidogo tita unapoligeuza.Kisha Peta ufuta wako na kuuweka katika Vyombo safi vya kuhifadhia.

Chanzo Mtandaoni

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa