Home » » Waandamana wakipinga kukatiwa mabomba ya maji

Waandamana wakipinga kukatiwa mabomba ya maji

WAKAZI wa kijiji cha Naisinyai wilayani Simanjiro mkoani Manyara wameandamana na kuzuia shughuli za utengenezaji barabara ya Kia-Mirerani, kwa kiwango cha lami wakidai kukatiwa mabomba ya maji.
Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 26 unaotekelezwa na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co Limited (Chico) ya China ni wa Sh bilioni 32.2 zinazolipwa na Serikali kwa asilimia 100.
Wananchi hao zaidi ya 300 wakizungumza juzi kwenye eneo hilo walidai kuwa ni zaidi ya miezi saba tangu mabomba yao ya maji yaharibiwe na matingatinga ya kampuni hiyo, hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa ili kuyatengeneza au kuyaunga ili waendelee kupata huduma ya maji.
Mmoja wa wakazi hao, Toima Makeseni, alisema anaendesha mradi wa kuosha magari kwenye eneo hilo, hivyo kukosekana kwa maji kutokana na kukatwa kwa mabomba hayo kumesababisha asimamishe kazi hiyo kwa muda huku akiendelea kudaiwa ushuru wa halmashauri na mapato mengine ya serikali.
“Ni muda mrefu tuliwaeleza kuhusu tatizo hilo ili watengeneze miundombinu ya maji waliyoiharibu lakini walituzungusha kwa miezi saba na kutufanya tukwame kuendesha shughuli zetu,” alisema.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa