Na. Abushehe Nondo na Immaculate Makilika- MAELEZO
Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman amesema kuwa Serikali inatarajia kuzindua mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa miaka 5 unaolenga kuboresha huduma za kimahakama nchini.
Aidha
Jaji Mkuu alisema uzinduzi wa mpango huo utaenda sambamba na mradi wa
maboresho wa huduma za utoaji haki nchini uliogharimu kiasi cha Tsh
Bilioni 140.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Jaji Chande alisema kuwa mradi huo una nguzo tatu ambazo ni utawala bora na uwajibikaji , fursa ya kutoa na kupata haki na uharakishaji wa mashahuri ambapo kwa pamoja umekusudia kutoa haki kwa wote na kwa wakati.
“Katika
kujenga imani ya wananchi kwa mahakama tunataka kufikia sehemu ambapo
mtu yeyote akileta shauri lake Mahakamani basi litasikilizwa kwa wakati”
alisema Jaji Chande.
Aliongeza
kuwa taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa asilimia 47 ya
Watanzania hawana fursa sawa ya kupata haki ya Mahakama katika maeneo
waliopo hususani mikoani kwa kuwa mikoa mingi haina Mahakama Kuu, hivyo
mpango huo utakaozinduliwa utalenga kuboresha utendaji na utoaji huduma
za kimahakama nchini.
Akizungumzia
kuhusu mradi wa maboresho ya huduma za Mahakama ambao unaandaliwa kwa
ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia Jaji Chande alisema kuwa mradi huo unalenga kuimarisha mifumo ndani ya Mahakama, kuendesha kesi na utoaji wa hukumu kwa wakati.
Jaji
Chande aliongeza kuwa mradi huo utapanua wigo wa utoaji huduma za
kimahakama ambapo itatoa fursa za mafunzo endelevu kwa watumishi wa
Mahakama 6400 wa ngazi mbalimbali.
Aidha alisema mpango huo utasaidia kuimarisha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kukijingea uwezo wa kutoa taaluma bora kwa watumishi pamoja na wadau katika masuala ya Sheria.
Jaji
Chande alisema tayari mradi huo umewezesha kujengwa kwa Mahakama tano
za kisasa zilizopo katika maeneo ya Kibaha, Kawe, Kisarawe, Kigamboni na
Bagamoyo ambazo zitakuwa mfano wa uanzishwaji wa Mahakama za kisasa nchini.
Mradi huo unaogharimu bilioni 140 utazinduliwa Kibaha mkoani Pwani Septemba 21 mwaka huu, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
0 comments:
Post a Comment