MTOTO Flora William wa kijiji cha Mandi wilayani Babati, Manyara
aliyezaliwa akiwa na ulemavu wa kutokuwa na sehemu ya haja kubwa,
ameendelea kuteseka kwa miaka 15 sasa kutokana na wazazi wake kutokuwa
na uwezo wa kuwezesha matibabu yake.
Licha ya kuteseka, amekuwa na wakati mgumu kutokana na kunyanyapaliwa
na watoto wenzake, sababu kubwa ikielezwa ni kutumia sehemu ya tumbo
kutoa haja kubwa.
Wazazi wa mtoto huyo, Stella Martin ambaye ni mama na mumewe William Philipo, wamezungumzia hali hiyo inayomkabili mtoto wao.
Stella, alisema alimzaa akiwa na hali hiyo na alipojaribu kumweleza
mama mkwe wake alimtaka asimwambie mtu yeyote, akidaiwa kusema itakuwa
aibu kuieleza jamii inayowazunguka kuwa mtoto huyo hana sehemu za haja
kubwa.
Alisema alijaribu kumsihi mume wake kumpeleka mtoto huyo hospitali
akiwa bado mdogo ili atibiwe na kubahatika kwenda katika Hospitali ya
Hai mkoani Manyara alikopata matibabu ya kupasuliwa sehemu za mbavu.
Alisema baadaye waliambiwa wampeleke mtoto huyo katika Hospitali ya
Rufaa ya KCMC iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi
ambako walitakiwa kugharimia Sh 200,000 ili mtoto aweze kutibiwa, lakini
hawakuwa na fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, mama huyo alisema walilazimisha kurejea
nyumbani ili kutafuta fedha zaidi, lakini hawakufanikiwa na hivyo
kuendelea kubaki na mtoto wao ambaye kwa sasa amekua na kufikisha umri
wa miaka 15.
Inaelezwa kuwa, hali ya mtoto huyo kadri anavyozidi kukua inazidi
kuwa mbaya kutokana na sehemu alizopasuliwa kwa ajili ya kutolea haja
kubwa tumboni kwake. Kwa mujibu wa mama wa mtoto huyo, kwa sasa utumbo
umetoka nje hivyo inamlazimu kujifunga tumboni mfuko mweusi wa Plastiki
wakati wa kujisaidia ili kuhifadhi kinyesi chake.
Baba mzazi wa mtoto huyo, alisema kwa sasa hana fedha za kumpeleka
mtoto huyo hospitali kutokana na kuwa na hali duni ya uchumi, hivyo
kuwaomba Watanzania wajitokeze kumsaidia aweze kumpeleka mwanawe huyo
hospitali.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment