Na Beatrice Lyimo-MAELEZO-
10/10/2016
SERIKALI imesema imejipanga kuhakikisha kuwa idadi kubwa ya wananchi waishio vijijini
na mijini hapa nchini wananufaika na huduma ya upatikanaji wa maji safi
na salama ili kuwaondolea kero ya uhaba wa maji watanzania ifikapo mwaka 2020.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge wakati wa uzinduzi wa Bodi ya
wadhamini ya Mfuko wa Maji.
Amesema
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuongeza huduma ya
upatikanaji wa maji vijijini kutoka asilimia 72 hadi asilimia 85 na
mijini kutoka asilimia 86 hadi asilimia 95 ifikapo mwaka 2020.
Waziri
Lwenge amesema ili kufikia lengo hilo Serikali itahakikisha
inafanyakazi kwa juhudi na weledi na maarifa ili kuondokana na kero
hizo.
“Katika
kufikia malengo ya Serikali kuwa ifikapo mwaka 2020 huduma ya maji
inawafikia wananchi waishio vijijini kwa asilimia 85 kutoka asilimia 72
ya sasa na mijini kwa asilimia 95 kutoka aslimia 86 ya sasa,” alifafanua
waziri Lwenge.
Katika
kufanikisha hilo Waziri Lwenge ameiagiza Bodi hiyo kuwa wabunifu,
waadilifu na wachapakazi ili kuleta mabadiliko ambayo yataiwezesha nchi
kuwa nchi ya Uchumi wa kati na ya Viwanda hasa katika Sekta ya Maji.
Kwa
upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mbogo Futakamba alisema
kuwa matumaini ya Serikali katika kuimarisha hali ya huduma ya maji
vijijini na mjini ni kuona mfuko huo unasimamia ili kutoa matunda
yaliyokusudia.
0 comments:
Post a Comment