Home » » TANZANIA YAPATA MKOPO WENYE MASHARTI NAFUU WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 300 KUTOKA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (afdb) NA SERIKALI YA KOREA

TANZANIA YAPATA MKOPO WENYE MASHARTI NAFUU WA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 300 KUTOKA BENKI YA MAENDELEO YA AFRIKA (afdb) NA SERIKALI YA KOREA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Benny Mwaipaja, WFM, Seoul, Korea
TANZANIA, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Korea ya Kusini zimetiliana saini makubaliano ya pamoja kutekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya umeme gridi ya Kaskazini Magharibi inayoanzia mkoani Mbeya, Nyakanazi hadi Kigoma, yenye msongo wa kV 400 mbapo Serikali ya Korea imeahidi kutoa Dola za Marekani milioni 50 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 100.18, kwa ajili ya kugharamia mradi huo.
Hali kadhalika, Tanzania na Benki ya Exim ya Korea, zimesaini  Mkataba wa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za marekani milioni 90.092 sawa na zaidi ya shilingi Bilioni 194 za Tanzania, kwa ajili ya mradi wa Upanuzi wa Miundombinu ya mfumo wa maji taka Jijini Dar es salaam.
Kwa upande wa Tanzania, Makubaliano pamoja na Mkataba vimesainiwa na Mhe. Dkt. Philip Mpango (MB) Waziri wa Fedha na Mipango kwa niaba ya Serikali, Oktoba 25, 2016 Jijini Seoul nchini Korea Kusini huku upande wa AfDB, aliye saini ni Rais wa Benki hiyo Adesina Akinwumi, na kwa upande wa Benki ya Exim, mkataba huo umesainiwa na Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Benki hiyo Lee Duk-Hoon.
Akizungumza mara baada ya kutia saini makubaliano na mkataba huo, Dkt. Mpango amesema makubaliano na mkataba vilivyosainiwa vina manufaa makubwa kwa wananchi wa Tanzania.
Pause ( Kwa TV) Waziri Mpango-akizungumza kuhusu umeme
“Wananchi wa Upande ule waanze kufurahia kwamba maendeleo yanakuja na hasa tunaposema maendeleo ya viwanda ambavyo ni lazima vitumie umeme, na kwamba mradi huu unatarajia kupelekwa hadi Mbeya” Amesisitiza Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango, amesema kuwa mradi huo una umuhimu mkubwa pia kwa kuwa serikali imedhamiria kuufungua ukanda wa Magharibi mwa Tanzania, kwa upande wa viwanda vya aina mbalimbali.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji (Uwekezaji) wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanzania-TANESCO, Decklan Mhaiki, amesema mradi wa umeme wa Nyakanazi hadi Kigoma utakuwa na urefu wa kilometa 280 na utakapo kamilika utaondoa changamoto ya shirika hilo kuzalisha umeme unatumika katika ukanda huo wa Magharibi hususan Kigoma, kwa kutumia majenereta ambayo uendeshaji wake ni ghali na umeme wake si wa uhakika.
Pause (kwa TV) Mhaiki Tanesco-Akizungumzia umuhimu wa mradi
“Kuleta laini kama hii, kwanza itapunguza gharama kubwa, na umeme wa ziada utakao zalishwa tunaweza kuuza nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, upande wa pili wa Ziwa Tanganyika, lakini kikubwa ni kuwahakikishia wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwa na umeme wa uhakika” ameongeza Bw. Mhaiki.
Akizungumzia mkataba wa ujenzi wa miundombinu ya maji taka Jijini Dar es salaam, Dkt. Philip Mpango, amebainisha kuwa mradi huo unatarajia kuwa na tija kwakuwa utatatua changamoto ya majitaka kutuama mitaani hasa wakati wa mvua na kusababisha magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Manyara Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za mikoa