Na MOHAMED HAMAD,
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamimu
Kambona, amesema hatawavumilia watumishi wa Serikali wilayani humo
watakaoshindwa kutimiza wajibu wao.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi ya ujenzi na umwagiliaji
yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 400 juzi, Kambona alisema baadhi ya
wakuu wa idara hawatimizi wajibu wao na kwamba njia pekee ni
kuwachukulia hatua za kinidhamu.
“Kuna watu wanashindwa kutimiza wajibu wao wakati wao ni watumishi wa
umma. Katika hili, nitaanza na ofisa kilimo wa wilaya ambaye ameshindwa
kuwajibika na kusababisha manung’uniko kwa wananchi.
“Watu kama hawa hatuna sababu ya kuwa nao humu, tumesema kila mtumishi awafikie wananchi walipo.
“Lakini jambo la ajabu ni kwamba, tangu tuzindue mradi wa maji zaidi
ya mwezi, katika Kijiji cha Orgira, hajautembelea mradi huo ili kuona
kinachoendelea wakati akijua umegharimu zaidi ya Sh milioni 160.
“Kwa hili nasema siko tayari kuvumilia, nitafanya kazi na wale ambao tutaendana nao katika kuwatumikia wananchi.
“Wale watakaoona hawana sababu ya kuwatumikia wananchi, waondoke iwe
ni kwa kuandika barua za kuacha kazi wenyewe au kwa namna yoyote
watakayoona inawafaa,” alisema Kambona.
Katika hatua nyingine, mkurugenzi huyo amelazimika kuweka makazi yake
kwa muda katika vijiji vya Sunya na Kijungu ili kusimamia kwa ukaribu
miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa manne na
vyoo katika Shule ya Sekondari Kijungi, vyoo na nyumba moja ya mwalimu
iliyoko katika Kijiji cha Sunya.
CHANZO GAZETI LA MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment