Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.
MAAFISA
Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kuacha kutumia muda mwingi kukaa
maofisini na badala yake kutembelea jamii inayowazunguka ili kubaini
fursa zitakazoleta mabadiliko ya haraka katika jamii.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Sihaba Nkinga wakati wa mahojiano
Maalum ya kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari
(MAELEZO) na kurushwa hewani na Shirika la Utangazaji Nchini (TBC).
Bi.
Sihaba amesema kuwa Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuanzisha Vyuo
vya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuzalisha maafisa wengi wa kada hiyo
watakaotumika kuisaidia Serikali katika kuibua fursa mbalimbali
zilizopo kwenye jamii ambazo zitasaidia kuleta maendeleo ya nchi.
“Afisa
Maendeleo ya Jamii ni chachu ya maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla
kwani wao ndio wana jukumu la kubaini fursa na kuwaongoza wananchi
katika kutumia fursa hizo,” alisema Bi. Sihaba.
Ameongeza
kuwa jukumu kubwa la maafisa maendeleo ni kuwahamasisha, kuwashirikisha
na kuwajengea uwezo wanajamii kutumia rasilimali walizonazo kujiletea
maendeleo yatakayopelekea kukua kwa uchumi wa nchi.
Aidha,
Bi. Sihaba amewataka wananchi kuacha dhana potofu ya kuitegemea
Serikali na badala yake washirikiane na Serikali kuleta maendeleo kwa
kufanya kazi kwa bidii kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka katika
maeneo wanayoishi.
Akiongelea
kuhusu makazi ya wazee, Bi. Sihaba amesema kuwa kwa sasa kuna vituo 17
nchi nzima vyenye jumla ya wazee 460 wanaopatiwa huduma mbalimbali
zikiwemo za malazi, mavazi na chakula.
“Tunatoa
rai kwa vijana kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujitegemea na sio
kwenda kukaa kwenye nyumba za wazee ili wapatiwe huduma, makazi ya wazee
ni kwa ajili ya wazee wasiojiweza tu,” alimalizia Bi. Sihaba.
0 comments:
Post a Comment