Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Joachim Mushi, Babati
Mkuu
wa Wilaya ya Babati, Raimond Mushi amewataka wakulima kufuata maelekezo
ya wataalamu wa kilimo wakiwemo watafiti wa mbegu bora chotara za
mahindi zinazostahimili ukame, magonjwa (WEMA) ili waweze kuendesha
kilimo chenye tija na kuachana na kilimo cha kujikimu ambacho hakiwezi
kuwapa maendeleo.
Alisema
kilimo cha sasa kinapaswa kuendeshwa kisayansi na kufuata ushauri wa
kitaalamu, ambapo ni pamoja na kutumia mbegu bora zilizofanyiwa utafiti
kulingana na mahitaji ya maeneo ya wakulima.
Mh.
Mushi ametoa ushauri huo mjini Babati alipokuwa mgeni rasmi kwenye
maadhimisho ya Siku ya Wakulima wilayani Babati ambapo pia alitembelea
shamba la utafiti shirikishi wa mbegu za mahindi unaotekelezwa na
watafiti kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano na Tume
ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia mradi wa utafiti wa
mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa (WEMA).
Alisema wakulima wakitaka kufanya kilimo cha manufaa hawana budi
kutumia mbegu zilizofanyiwa utafiti na kupendekezwa na wataalamu wa
kilimo kutumika katika maeneo yao.
"...Tuwe
macho na mbegu tunazonunua ili tuweze kuvuna mazao ya kutosha, wakulima
sasa lazima tubadilike tusiendeshe kilimo cha kujikimu tu...mkulima
huwezi kuendelea kwa kufanya kilimo cha kujikimu, tunataka ulime upate
chakula na ziada kisha uuze mazao kukuza uchumi wako na ubaki na akiba,"
alisema Raimond Mushi. Alisema serikali ya awamu ya nne imedhamiria
kufanya uchumi wa viwanda hivyo wakulima wanakila sababu ya kufanyia
kazi ushauri wa wataalamu wa kilimo ili waweze kuzalisha mazao ya
kutosha yatakayotumika kama mazao ghafi kwenye viwanda na kunufaika
zaidi.
"Tunapolima
sasa tulime kisayansi na kwa malengo, tutumie maeneo yetu vizuri ili
tuweze kuzalisha mazao ya kutosha," alisisitiza Mkuu wa Wilaya, Raimond
Mushi na kuongeza eneo la kilimo kwa sasa linapungua kutokana na
ongezeko la idadi ya watu nchini hivyo kuna kila sababu ya kutumia eneo
dogo linaloleta matokeo makubwa na manufaa kwa mkulima. Alisema serikali
imedhamiria kuleta mabadiliko kwa wakulima ndio maana inawawezesha
wataalamu kama WEMA na kuwaunga mkono shughuli za utafiti kwa maendeleo
ya wananchi hawa wakulima.
"Sisi
hapa Babati tunangoja kwa hamu matokeo ya utafiti ili tuweze kuyafanyia
kazi...tuleteeni mapema tutasimamia na kuhamasisha wakulima wetu
kutumia mbegu za WEMA," alisema. Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa
Kitengo cha Maendeleo ya Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Mifugo na
Uvuvi, Jackson Nkuba alisema Serikali ipo tayari kushirikiana na
makampuni yatakayojitokeza kuzalisha mbegu za WEMA na zingine bora
zinazofanyiwa utafiti ili wakulima wazipate kirahisi, hivyo kutoa rai
kujitokeza kwa wingi.
Awali
Mkuu wa Wilaya ya Babati, Bw. Mushi, viongozi mbalimbali katika tukio
hilo wakiwemo wakulima kwa pamoja walitembelea shamba la utafiti
shirikishi wa mbegu bora chotara za mahindi zinazostahimili ukame na
magonjwa (WEMA) lililopo Mtaa wa Maisala Kata ya Babati Mjini na
kujionea mbegu zilizofanyiwa utafiti wa WEMA na kujionea matokeo ya
utafiti.
0 comments:
Post a Comment