Serikali kupitia Mfuko
wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea na kazi ya kuhakikisha kuwa wanachi wote
waishio vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara wanapata huduma za
mawasiliano kwa wakati ili kuweza kuchangia ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa
huduma za kijamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na
Mtendajii Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga
wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu ya kukagua ujenzi
wa minara ya simu za mkononi na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye
maeneo mbalimbali vijijini ya mkoa wa Arusha na Manyara. Eng. Ulanga amesema kuwa migogoro ya ardhi
kwenye baadhi ya vijiji mbalimbali nchini inachangia ucheleweshaji wa ujenzi wa
minara na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mfuko huu uliweka lengo la kufikisha
mawasiliano kwenye vijiji 4,000 nchi nzima ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.
Uwepo wa migogoro ya ardhi unachangia kuchelewesha kampuni za simu zilizopatiwa
ruzuku na Serikali kujenga minara, “mgogoro wa ardhi kwenye kijiji cha Timbolo
kata ya Sambasha Wilayani Arumeru
umeichelewesha kampuni ya Halotel kujenga mnara na hivyo wananchi wa kata hii
kukosa mawasiliano kwa kuwa mgogoro huo umechukua zaidi ya miaka miwili
kukamilika mahakamani,”amesema Eng. Ulanga.
Kaimu Mkurugenzi wa
kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Arusha Bwana Philemon Joel amesema kuwa
mahakama iliweka zuio la ujenzi wa mnara kwenye eneo la kijiji cha Timbolo kata
ya Sambasha ambapo kesi ya mgogoro huo umechukua miaka miwili kufanyiwa maamuzi
kwenye ngazi ya mahakama. “Tumekuwa tukienda mahakamani mara kwa mara na
kupigwa tarehe kuambiwa Hakimu hayupo na mara nyingine inapita miezi minne bila
ya kesi kusikilizwa hivyo imetuchelewesha kuanza ujenzi,”amesema Bwana Joel.
Naye Mwenyekiti wa
kijiji cha Timbolo, kata ya Sambasha Bwana Samwel Saning’o amesema kuwa Serikali
ya kijiji ilisimama na kusema kuwa wanataka mawasiliano na sio utalii kwa kuwa
kulikuwa na mgogoro baina ya mmiliki wa eneo la jirani na eneo la mwingine
ambapo mnara unatakiwa kujengwa. Bwana
Saning’o amemshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Bwana Alexandra Mnyeti kwa
kuingilia kati mgogoro huu, kusimamia na kuhakikisha kuwa unakamilika ili
wananchi waweze kupata mawasiliano. Eng. Ulanga amesema ujenzi wa mnara wa
Halotel kwenye eneo hili hauwezi kukamilika mwezi Novemba mwaka huu, hivyo sisi
kama Mfuko wa UCSAF tutawapatia muda wa ziada ili waweze kukamilisha ujenzi wa mnara
na wananchi waweze kupata mawasiliano. Pia Eng. Ulanga amewataka wanachi wa
vijiji husika kushirikiana na kampuni za simu kulinda miundombinu ya
mawasiliano na minara ili mawasiliano yaweze kupatikana muda wote.
Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King ametoa rai kwa mamlaka
zinazosimamia haki na vyombo vya ulinzi viambata vya Jeshi la Polisi na
mahakama kufanya uchunguzi na kuendesha kesi kwa wakati ili kuharakisha kutoa
haki. “Ukichelewa kutoa shauri la hukumu kwa jambo la umma linalogusa maslahi
ya wananchi unachelewesha maendeleo ya wananchi,”amesema Prof. Norman Sigalla
King. Ameongeza kuwa wananchi washirikiane na kampuni za simu za mkononi
kulinda minara na kutoa ardhi bila migogoro ili waweze kupata huduma za mawasiliano
kwenye vijiji vyao kwa wakati.
Katika hatua nyingine,
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King ameitaka
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kukamilisha ujenzi wa minara yake ya simu kwa
wakati kwenye vijiji mbalimbali nchini ili wananchi wa maeneo husika waweze
kupata huduma za mawasiliano. Hayo ameyasema Prof. Norman Sigalla King wakati
wa ziara ya Kamati yake walipotembelea kijiji cha Sigino kata ya Singo iliyopo
wilaya ya Babati Mjini mkoani Manyara.
Naye Meneja wa TTCL
Mkoa wa Arusha na Manyara Bwana Brown Japhet amesema kuwa TTCL imekamilisha
ujenzi wa minara kwenye vituo vyote vya Mkoa wa Arusha na viko hewani wananchi
wanapata mawasiliano. Bwana Japhet ameilieza Kamati kuwa kwa vituo viwili
vilivyobaki vya TTCL kama pale Saitabau, Arusha kulikuwa na mgogoro wa ardhi ambapo
Serikali ya Mkoa imeingilia kati na kumaliza mgogoro huo na vituo vingine viwili
vipo kwenye hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambapo vinasubiri tathmini ya
mazingira ikamilike ili ujenzi wa minara kwenye vituo hivyo uweze kuanza na
suala hili limefikishwa Wizara ya Maliasili na Utalii ili liweze kukamilishwa.
Prof. Norman Sigalla King
ameyataka makampuni ya simu kuhakikisha kuwa mawasiliano yanasambaa nchi nzima.
Pia ameitaka TTCL kukamilisha ujenzi wa minara yake kwa wakati na kuhakikisha
kuwa kila wanapopatiwa ruzuku na Serikali wakamilishe jukumu lao kwa wakati na
wafanye kazi kwa ushindani. Ameoneza kuwa Kamati yake imeridhishwa na kazi
nzuri inayofanywa na TTCL. Kamati inazitaka mamlaka nyingine zinazohusika na
ujenzi wa minara na upatikanaji wa mawasiliano vijijini washirikiane kwa pamoja
na kufanya maamuzi kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za
mawasiliano vijijini kwa wakati.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 comments:
Post a Comment